TANGU mwaka huu uanze kumekuwa na matukio mengi yaliyojitokeza kwa mastaa, ambayo yalileta mshtuko kwenye jamii hususan kwa watu wanaofuatilia masuala ya burudani kwa wasanii, hapa nakuorodheshea matukio hayo.
1.MAKONDA KUWATUMBUA MASTAA ISHU YA DAWA ZA KULEVYA
Ni ishu iliyokuwa gumzo jijini kufutokana na Mkuu wa Mkoa wa Dar, Paul Makonda kuwatumbua baadhi ya wasanii kwa kuwataja majina na kuwaita Kituo Kikuu cha Polisi kutokana na kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya. Miongoni mwa wasanii waliokuwepo kwenye orodha hiyo ni Wema Sepetu, Lulu Abbas ‘Lulu Diva’, Recho kizunguzungu, TID, Petitman, Deogratius Shija, Salma Jabu Nisha, Tunda Sebastian na wengine wengi.
2.WEMA KUHAMA CHAMA
Mwanadada huyu alikuwa mstari wa mbele kwenye Chama Cha Mapinduzi (CCM), hususan kwenye kampeni ya ‘mama ongea na mwanao’ ambayo ilikuwa ikiendeshwa katika kipindi cha uchaguzi, wakimsapoti Makamu wa Rais mama Samia Suluhu Hassan. Lakini ghafla baada ya Wema kupata msala wa kutumia dawa hizo alihama chama hicho na kuhamia Chadema kwa kuhisi CCM ilimtenga baada ya kupata tatizo hilo.
3. NAY KUWEKWA NDANI
Ilikuwa kizaazaa pale mwanamuziki Emanuel Elibarick alipowekwa ndani baada ya kutoa wimbo uitwao Wapo ambao ulionekana kuwakashifu baadhi ya viongozi wa kiserikali. Hata hivyo, ilikuwa ni kauli moja tu ya Rais Dk John Magufuli aliyesema aachiwe na ikawa hivyo. Mwanamuziki huyo alikaa ndani siku moja.
4.ROMA KUTEKWA
Nchi nzima ilizizima kutokana na mwanamuziki wa Hip Hop, Ibrahimu Mussa ‘Roma Mkatoliki’ kutekwa pamoja na mwanamuziki Moni Central Zone na kijana mwingine ambaye alikuwepo studio hapo Tongwe Record, gumzo hilo liliendelea hadi walipopatikana huku kila mmoja akizungumza lake kuhusu nani alifanya utekaji huo.
5. NUH KUACHANA NA NAWAL
Wengi hawakuamini kilichotokea wakawa wanahisi ni kiki baada ya mwanamuziki Nuh Mziwanda kubwagana na mkewe Nawal ambaye amebahatika kupata naye mtoto mmoja Anya. Lakini huo ndiyo ulikuwa ukweli maana baadaye mwanadada huyo alifunga ndoa na mtu mwingine.
6. HARUSI YA JOTI
Taarifa za harusi hiyo zilipoanza kuenea watu walifikiri ni utani. Lakini baadaye Joti na mkewe walipoonekana wakiwa kanisani na picha kutoka vikiwemo vipande vya video huku mitandao ya kijamii ikienea habari zake, kila mmoja aliamini kweli Joti amefunga ndoa na mkewe.
7. BIFU LA HAMISA NA ZARI
Hili ni miongoni mwa matukio yaliyobamba mwaka huu. Bifu hili liliibuka baada ya mwanamitindo Hamisa Mobeto kuweka wazi kwamba alizaa na Mbongo Fleva ambaye ni mzazi mwenza na mjasiriamali Zarinnah Hassan ‘Zari Ze Bossy Lady.” Hata hivyo, baada ya vijembe mitandaoni baadaye suala hili lilionekana la kawaida na kupitwa na wakati.
8. NDOA YA UWOYA NA DOGO JANJA
Taarifa za muigizaji Irene Uwoya kufunga ndoa na Mbongo Fleva, Dogo Janja ziliwashangaza wengi. Ikawa gumzo kubwa ambalo baadaye lilikosa tija baada ya Uwoya kuweka wazi kupitia magazeti ya Global Publishers kwamba hakufunga ndoa bali ni muvi inayotarajiwa kutoka.
9. LULU KUTUPWA JELA
Tukio la muigizaji Elizabeth Michael ‘Lulu’ kuhukumiwa kwenda jela kwa muda wa miaka miwili kutokana na kesi ya kumuua bila kukusudia muigizaji Steven Kanumba ilikuwa ni gumzo mpya kwenye media (vyombo vya habari). Wengi hawakuamini kama Lulu angeweza kwenda jela, lakini sheria ni msumeno na hivi tunavyozungumza Lulu yupo jela Seregea.
10. DK SHIKA NA ITAPENDEZA
Hadi sasa hili ndilo tukio la funga mwaka. Tukio hili limebamba baada ya kuibuka mzee mmoja aliyevaa nguo za kawaida na sandozi zilizochoka mguuni akitaka kununua nyumba za Saidi Lugumi.
Mzee huyo si mwingine bali Dokta Loius Shika ambaye alijizolea umaarufu kwenye mnada huo na msemo wa ‘mia tisa itapendeza’ na kuweka wazi kwamba ana mabilioni ya pesa kwenye benki tofauti tofauti nje ya nchi, kwa sasa mzee huyo anakula madili ya matangazo likiwemo kutoka Kampuni ya Sokabet.
No comments:
Post a Comment