Azam FC itakuwa imetibu lile suala lake la ushambulizi na kuhakikisha inapata mabao mengi zaidi.
Hii inatokana na ruhusa waliyoipata ya kumtumia straika wake mpya, Bernard Arthur raia wa Ghana baada ya kukamilisha taratibu zote za usajili ikiwemo kuwasili kwa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC).
Azam imemsajili straika huyo kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Klabu ya Liberty Proffessionals ya nchini Ghana ili kuchukua nafasi ya Mghana mwenzake, Yahaya Mohammed aliyefungashiwa virago hivi karibuni.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas, alisema walitoa ruhusa ya mchezaji huyo kuanza kuitumikia Azam kabla hata ya mchezo wao wa juzi Jumatatu wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa Sugar.
“Hivi sasa Azam inaweza kumtumia straika wao mpya kwani wamekamilisha kila kitu kinachotakiwa kufanyika ikiwemo kuwasili kwa ITC yake.
“Hivi sasa mchezaji akisajiliwa kisha taratibu zikafanyika haraka, basi sisi tunamruhusu kuanza kuitumikia timu yake mpya wakati usajili ukiendelea,” alisema Lucas.
No comments:
Post a Comment