Thursday 30 November 2017

Waombolezaji watelekeza jeneza



HALI ya taharuki na hofu imezuka katika Kijiji cha Katani Kata ya Nkandasi wilayani Nkasi mkoani Rukwa na kusababisha waombolezaji kutimua mbio na kuacha jeneza lenye mwili wa marehemu baada ya mvua kubwa kuanza kunyesha na kubomoa nyumba za wakazi wa kijiji hicho.

Tukio hilo lilitokea jana saa 6 mchana baada ya kuanza kunyesha mvua kubwa iliyoambatana na radi na upepo mkali ulioezua baadhi ya nyumba za wananchi hao ambao walikuwa wakiomboleza msiba wa mwananchi mwenzao aliyefariki baada ya kuugua siku chache zilizopita.

Mwenyekiti wa serikali ya kitongoji cha Kaungo, Robert Kanoni, alisema wakiwa wanaelekea kufanya maziko ya marehemu Dismas Kanoni aliyefariki jana, ghafla ilianza kunyesha mvua kubwa ikiambatana na radi na upepo mkali hali iliyosababisha baadhi ya waombolezaji kutimua mbio na kurejea majumbani kutokana na hofu iliyoibuka kufuatia tukio hilo.

Baadhi ya wananchi walivumilia nakurejea na jeneza lililokuwa na mwili wa marehemu nyumbani na kuahilisha maziko kwa muda ili kupisha hali hiyo itulie na walikwenda kuzika baadaye katika makaburi yaliyopo kijijini hapo.

Alisema tukio hilo limezua hisia za kishirikina kwa wananchi wa kijiji hicho kwani miezi miwili iliyopita baba yake na marehemu huyo alifariki baada ya kugongwa na gari la kampuni ya ujenzi wa barabara na walipofanya maziko siku iliyofuata walikuta ngozi ya kondoo juu ya kaburi la marehemu kitendo kilichowashangaza.

Kanoni alisema kutokana na mvua hiyo, nyumba zipatazo 10 zimebomoka kabisa na zinatakiwa kujengwa upya huku makazi licha ya kuwa wamepata hifadhi na misaada ya kibinadamu kwa wenzao. 

Naye Peter Kalale, mkazi wa kijiji hicho akizungumzia tukio hilo, alisema mara kwa mara kijiji hicho kimekuwa kikikumbwa na dhoruba pindi mvua zinaponyesha kwa kuwa kimepitiwa na mkondo wa upepo mkali ambao unasababisha hali hiyo.

Alisema changamoto iliyopo ni tabia ya wananchi kukata miti kwa ajili ya mashamba hivyo kusababisha pepo zinapovuma hazikuti kizuizi chochote na kuwa sababu ya kuezuliwa nyumba zao na wakati mwingine kubomoka kabisa.

Mwenyekiti wa kamati ya maafa ya wilaya hiyo ambaye ni Mkuu wa wilaya  hiyo, Said Mtanda, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kutoa wito kwa wananchi kujenga makazi bora kwani miongoni mwa nyumba  hizo zipo ambazo zimeezekwa kwa nyasi.

Alisema sera ya serikali ya awamu ya tano ni kuwahimiza wananchi wajenge nyumba bora na za kisasa ili waepuke majanga yanayotokana na tabianchi kwani bila kufanya hivyo, wananchi wataendelea kupata hasara.

No comments:

Post a Comment