Friday, 1 December 2017

Dr. Shika aandaliwa tamasha la ‘Usiku wa 900 itapendeza’




Dkt. Louis Shika ambaye amejizolea umaarufu baada ya kuibuka mshindi katika mnada wa nyumba za mfanyabiashara maarufu, Said Lugumi, na kushindwa kuzilipia, ameandaliwa usiku wake maalum ambao ataongea na Watanzania juu ya maisha yake.

Akizungumza na waandishi wa Habari mapema jana  Novemba 30, 2017, Jijini Dar es Salaam, Meneja wa Dkt. Shika, Catherine Kahabi aliweka wazi kuwa wamekuja na wazo hilo la kuandaa tamasha maalum ili watu wote wamtambue Dkt. Shika kama mmoja wa watu wakubwa ambao wameweza kuibuka katika mazingira ya chini na baadae kuwa gumzo kila kona.

“Usiku wa 900 Itapendeza ni usiku maalum ambao unatarajiwa kufanyika Desemba 9, mwaka huu. Watu wote wanakaribishwa pale ndani ya uwanja wa burudani, Dar  live. Usiku huo ni maalum na Dkt. Shika ataweka wazi kila kitu pamoja na historia yake alianzia wapi mpaka kufika Nchini Urusi na baadae kurejea Tanzania” amesema Catherine

Pia aliongeza kuwa, kwa sasa wanamuangalia Dkt. Shika kama ni mmoja wa Watanzania wenye bahati na muonekano wa tofauti licha ya kila mmoja kusema lake.

Mbali na Dkt. Shika, kutakuwa na burudani mbalimbali zitakazosindikizwa na bendi ya Twanga Pepeta, Jahazi Modern Taarab na wasanii wengine kibao wakiwemo wa Bongo fleva na wachekeshaji akiwemo MC Pilipili.

Kwa upande wake msimamizi wa masuala ya burudani wa Dar Live, Rajabu Mteta (KP Mjomba) amesemakuwa usiku huo utapambwa na shamrashamra mbalimbali kwani utakuwa ni wa aina yake kwa kila mmoja atakayefika siku hiyo.

“Wengi bado wapo njia panda kuhusiana na ukweli wa mabilioni ya Dkt. Shika, tumeshuhudia hivi karibuni amelipia bima fedha zilizopo nje ya nchi. Kabla fedha hizo hazijatua ameona awashangaze wananchi ambapo ukija Dar Live utaishuhudia,” amesema Mteta  KP Mjomba.

Usiku huo pia unatarajiwa kuwa na mgeni rasmi ambaye atafungua halfa hiyo, Mkurugenzi wa Global Group, Erick Shigongo kama mtu aliyemsaidia kwa namna moja ama nyingine Dkt. Shika.

No comments:

Post a Comment