Thursday, 30 November 2017

Diwani wa CCM afariki ajalini



Songea. Diwani wa viti maalumu (CCM), Mariam Yusuph (53) amefariki dunia katika ajali iliyojeruhi wengine wawili mkoani Ruvuma.

Ajali ilitokea walipokuwa wanakwenda kwenye uchaguzi wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Mkoa wa Ruvuma.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Songea, Dk Magafu Majura amesema amepokea majeruhi wawili na mwili wa diwani huyo leo Alhamisi Novemba 30,2017 saa 3:30 asubuhi.

Amesema majeruhi waliowapokea ni Asia Sapwela (52) ambaye ni diwani wa viti maalumu aliyevunjika mkono wa kulia, mbavu na ana michubuko miguuni.

Dk Majura amesema majeruhi mwingine ni Atingala Ally (48), ambaye ni diwani mstaafu wa Tunduru aliyeumia mbavu na mguu wa kulia. Amesema majeruhi wanaendelea na matibabu hospitalini hapo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Gemini Mushi akizungumzia ajali hiyo amesema imetokea katika Kijiji cha Lumecha wilayani Songea ikihusisha gari aina ya Toyota Carina.

Amesema gari hilo lilikuwa likitokea wilayani Tunduru kwenda Songea.

Kamanda Mushi amesema gari hilo likiendeshwa na Osam Ulaya liligonga kingo za barabara kabla ya kupinduka.

Amesema Mariam alifariki dunia papo hapo baada ya kujigonga kichwani.

Dereva Ulaya amepelekwa katika Hospitali ya Peramiho kwa matibabu na polisi wanaendelea na uchunguzi wa ajali hiyo.

No comments:

Post a Comment