Friday, 1 December 2017

Mabadiliko ya Simba yasimamisha usajili



WAKATI wanachama wa Klabu ya Simba wakitarajiwa kupewa taarifa kuhusiana na mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu hiyo ulivyofikia hapo keshokutwa, mkutano huo unadaiwa kusimamisha mchakato wa usajili, imeelezwa.

Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo inayodhaminiwa na Kampuni ya michezo ya kubashiri ya Sportpesa zinasema kuwa, mfanyabiashara maarufu, Mohammed Dewji "Mo" amesitisha kutoa fedha za kusajili wachezaji kutokana na mabadiliko ambayo yanaweza kufanyika tofauti na ilivyopendekezwa hapo awali.

Chanzo chetu kimesema kuwa kwa sasa mazungumzo yote ya kusajili wachezaji yamesimama kwa sababu bilionea huyo amekuwa na wasiwasi huenda mchakato huo hautafanikiwa.

"Kwa mfano suala la Mavugo (Laudit) kutolewa kwa mkopo lilianza kuzungumzwa lakini sasa halieleweki kwa sababu wanaogopa kumuuza na hawajui mbadala wake atapatikana vipi," kilisema chanzo chetu.

Kiliongeza kuwa hata mabadiliko ya asilimia ambazo wawekezaji wataruhusiwa kununua na zile zitakazobakia kwa wanachama zimeonekana kutowafurahisha baadhi ya viongozi na wadau ambao walikuwa tayari kuwekeza fedha zao ndani ya klabu hiyo.

"Simba imekuwa makini sana katika kufanya uamuzi wa masuala mbalimbali hasa ya matumizi ya fedha katika kipindi hiki, wanajipanga kujenga taasisi yenye nidhamu na inayojiendesha kisasa kwa sababu inataka kuonyesha mabadiliko huku pia ikiweka rekodi nzuri uwanjani," alisema kiongozi huyo.

Awali kabla ya kufanyika kwa tathmini, Mo alisema yuko tayari kupewa hisa asilimia 51 kwa thamani ya Sh. bilioni 20 na inadaiwa baadhi ya wafanyabiashara wengine walijitokeza ambao wameahidi kutoa fedha zaidi ya hiyo iliyotajwa na mfanyabiashara huyo wa hapa nchini.

Wakati huo huo wachezaji wa Simba wamepewa likizo ya wiki moja na watarejea tena uwanjani kuendelea kujiandaa kwa ajili ya kushiriki mashindano ya Kombe la Mapinduzi ambayo yatafanyika kuanzia Desemba 30 mwaka huu Zanzibar.

Source: Nipashe

No comments:

Post a Comment