Ripoti ya kituo cha sheria na haki za binadamu nchini Tanzania inaonesha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu umetekelezwa na vyombo vya dola katika uchaguzi mdogo wa udiwani uliofanyika nchini katika kata 43.
Ripoti hiyo inasema kuwa viongozi wa vyama vya siasa, wakala wa uchaguzi pamoja na baadhi ya wapiga kura walipigwa na wengine kuwekwa kizuizini wakati wakitekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria katika uchaguzi huo, hatua ambayo imeonesha hali ya wasiwasi katika uchaguzi unaokuja wa serikali za mitaa na uchaguzi Mkuu wa 2020.
Uchaguzi ulifanyika katika kata 43 zilizo kwenye halmashauri 36 za mikoa 19 nchini.
Akizungumza leo Alhamisi Novemba 30,2017 Kaimu Mtendaji Mkuu wa LHRC, Anna Henga amesema uchaguzi ulikuwa na matumizi mabaya ya vyombo vya dola, watu kupigwa, kukamatwa na kujeruhiwa.
"Vitendo hivi vimeripotiwa kufanywa na vyombo vya dola, watu wasiojulikana na watu wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa vyama vya siasa vikiwemo CCM na Chadema,” amesema.
Amesema kutokana na matukio hayo, vyombo vya dola vinapaswa kufanya uchunguzi wa kina na kuchukua hatua kali za kisheria kwa watakaobainika kuhusika kwa njia moja au nyingine.
Henga amesema matukio hayo yasipokemewa ni kiashiria kibaya na msingi mbaya utakaoathiri chaguzi zingine ukiwemo wa Serikali za Mitaa wa 2019 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
No comments:
Post a Comment