Kocha Mkuu wa timu ya mpira wa miguu ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, Ammy Conrad Ninje, ameongeza nyota watatu katika kikosi chake baada ya Baraza la Soka la Afrika Mashariki (CECAFA), kuridhia kuongezwa wachezaji watatu kwa kila timu.
Awali CECAFA ilihitaji wachezaji 20 tu, lakini sasa wameongeza watatu na kufanya idadi mpya ya wachezaji watakaoshiriki michuano hiyo ya Chalenji kwa mwaka huu kuwa 23. Wachezaji walioongezwa ni Kipa Ramadhani Kabwili kutoka Yanga, Amani Kiata wa Nakuru All Stars ya Kenya na Yahya Zayd kutoka Azam FC.
Wachezaji 20 walioitwa awali na kocha Ninje ni makipa Aishi Manula (Simba SC) na Peter Manyika (Singida United). Walinzi ni Gadiel Michael (Young Africans), Boniphace Maganga (Mbao FC), Kelvin Yondani (Young Africans), Kennedy Juma (Singida United), Erasto Nyoni (Simba SC) na Mohammed Hussein (Simba SC).
Viungo wa kati ni Himid Mao ambaye ni Nahodha (Azam FC), Jonas Mkude (Simba SC), Hamis Abdallah (Sony Sugar/Kenya), Mzamiru Yassin (Simba SC), Raphael Daud (Young Africans), Shizza Kichuya (Simba SC), Abdul Hilal (Tusker/Kenya) na Ibrahim Ajib (Young Africans). Washambuliaji ni Mbaraka Yussuph (Azam FC), Elias Maguri (Dhofar/Mascat, Oman), Daniel Lyanga (Fanja FC/Mascat) na Yohana Mkomola (Ngorongoro Heroes).
Katika michuano hiyo inayotarajiwa kuanza Desemba 3, mwaka huu, Kilimanjaro Stars imepangwa Kundi A pamoja wenyeji Kenya, Rwanda na Libya ambayo ni timu mwalikwa kutoka Kaskazini mwa Afrika. Kilimanjaro Stars imewahi kutwaa mara tatu taji hilo tangu kuanzishwa kwake.
No comments:
Post a Comment