Friday, 1 December 2017

Umeme wakatika karibia nchi nzima kuanzia jana



Dar es Salaam. Wakati umeme ukiwa umekatika nchi nzima kuanzia jana Alhamis, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limesema huduma hiyo imeanza kurejea kwenye mikoa ya Iringa, Dodoma na Tanga.

Akizungumza leo Ijumaa, Desema 1, 2017, Kaimu Meneja Mawasiliano wa Tanesco, Leila Mhaji amesema umeme umekatika katika mikoa yote iliyounganishwa katika gridi ya Taifa.

Amesema wataalam wa shirika hilo wanaendelea kurekebisha mifumo ya gridi ya Taifa ili kufanya matengenezo ya hitilafu iliyotokea.

“Marekebisho ya mafundi wetu yamesababisha umeme kurejea katika mikoa ya Iringa, Dodoma na Tanga,” amesema.

Amesema wataalam wamegundua mfumo wa gridi haujatengemaa vizuri na hivyo wanaendelea na kazi ya kurekebisha usiku na mchana ili kuhakikisha huduma hiyo inarejea katika hali yake ya kawaida.

“Tutaendelea kuwapa taarifa na tunaomba radhi kwa usumbufu utakaojitokeza,” amesema.

Amewatahadharisha wananchi kutokushika wala kukanyaga nyaya zilizokatika au kuanguka kwa kuwa ni hatari.

Ameitaja mikoa ambayo umeme haujakatika kuwa ni Kagera na Ruvuma ambayo haijaunganishwa na gridi ya Taifa.

No comments:

Post a Comment