Wednesday 29 November 2017

Wakulima Kilombero wametakiwa kutumia Viwanda kuongeza thamani ya Mazao


Wakazi wa Wilaya ya Kilombero wametakiwa kutumia viwanda vilivyopo kuongeza thamani mazao wanayozalisha na kuyauza.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, Denis Londo alitoa rai hiyo jana wakati akizindua kiwanda cha kati cha kukoboa, kupanga madaraja na kuuza mchele (Jatu) katika Kijiji cha Igima.

Alisema ujio wa kiwanda hicho ambacho kipo karibu na mashamba ya wakulima wa mpunga ni neema kwa kuwa malighafi zinapatikana kwa urahisi na kutawezesha kunufaika kwa kuuza ziada ya chakula.

Kwa mwaka jana pekee wilaya hiyo ilipata wastani wa mazao mchanganyiko tani 572,000 wakati mahitaji yalikuwa ni tani 138,0000 hivyo kuvuka lengo.

Londo alisema kuanzishwa kwa kiwanda hicho cha kati ni juhudi za Serikali za kutaka kila Mkoa kuhakikisha inafikisha viwanda 100, agizo lililotolewa hivi karibuni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Selemani Jaffo.

Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Petter Isare alisema baada ya kuhitimu masomo ya sheria ya elimu ya juu, waliamua kuanzisha asasi iliyolenga kutoa msaada wa kisheria na katika majukumu yao, wakagundua sehemu kubwa ya waliohitaji ni kutoka kundi la watu maskini wa kipato.

Isare alisema ndipo wakaamua kuangalia namna ya kusaidia kundi kubwa hilo kiuchumi na kiafya kwa wakati mmoja kwa kupitia fursa ya mazao mchanganyiko ndipo wakaanzisha kiwanda hicho.

Mwenyekiti wa kijiji cha Igima Timothy Mwakitalu alisema licha ya kusogea kwa kiwanda hicho kitakachosaidia pia kuhifadhi bure mazao kwenye ghala, kuna changamoto ya barabara.


No comments:

Post a Comment