Wednesday 29 November 2017

Atupwa jela miaka 10 kwa kukutwa na bastola




MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imemhukumu mfanyabiashara Gairo Mtozoma (43) kwenda kutumikia kifungo cha miaka 10 jela baada ya kukutwa na hatia ya mashtaka mawili, likiwamo la kupatikana na bastola kinyume cha sheria.

Pia Mtozoma alipatikana na hatia ya kukutwa na risasi kinyume cha sheria.

Mtozoma ambaye ni, mkazi wa Magomeni Kagera, jijini Dar es Salaam, alihukumiwa jana na Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa.

Akisoma hukumu hiyo, hakimu Mwambapa alisema baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na pande zote mbili, amejiridhisha kuwa bila kuacha shaka upande wa Jamhuri umethibitisha makosa dhidi ya mshtakiwa.Alisema kutokana na ushahidi huo, mahakama yake inamtia mshtakiwa hatiani.

"Mahakama hii baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi watano wa Jamhuri, imemwona mshtakiwa ana hatia na inamhukumu kwenda jela miaka 10," alisema hakimu Mwambapa. "Kosa la kwanza atatumikia miaka mitano na la pili, atatumikia mitano mingine."

Mapema mahakamani hapo upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga uliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa iwe fundisho kwa wengine.

Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa Agosti 11, mwaka jana katika eneo la Magomeni Kagera wilayani Kinondoni, jijini Dar es Salaam, Mtozoma alikutwa na bastola moja aina ya Browing yenye kumbukumbu  namba 90002 iliyosajiliwa kwa namba TZCAR-A222683 bila kuwa na leseni.

Pia ilidaiwa kuwa Agosti 11,2016 katika maeneo ya Magomeni Kagera wilayani Kinondoni alikutwa na risasi sita bila kuwa na leseni.

No comments:

Post a Comment