Monday 27 November 2017

Butiku aitaka Serikali Izingatie fidia kwa wanaobomolewa



Mwanasiasa mkongwe nchini, Joseph Butiku amesema wakati Serikali inatekeleza miradi yake mikubwa, kama ujenzi wa miundombinu, izingatie suala la fidia kwa wananchi wanaotakiwa kupisha miradi.

Amesema hayo wakati wakazi wa maeneo kadhaa nchini, hasa Ubungo hadi Kibaha, wakibomolewa nyumba zao kupisha upanuzi wa Barabara ya Morogoro huku wengine wakipisha ujenzi wa reli pana.

Katika maeneo mengi, wananchi hawajalipwa fidia kwa maelezo kuwa wamejenga ndani ya hifadhi ya barabara, wakiwemo wakazi wa Kimara hadi Kiluvya ambao wamebomolewa kwa kuzingatia utashi wa sheria ya kabla ya nchi kupata uhuru.

Akizungumza katika mahojiano na Mwananchi mwishoni mwa wiki, Butiku, ambaye alikuwa msaidizi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alisema ni lazima jitihada za Serikali zielekezwe katika kufanya mambo yanayowaridhisha wananchi na yanayowajengea amani.

“Kwa mfano, juzi kuna mtu aliniuliza kuhusu bomobomoa, nikasema itaendelea. Kwa nini, kwa sababu barabara tunataka kupanua, mabwawa ya maji yanataka kuchimbwa, reli tunataka kujenga, maeneo ya kucheza watoto yawepo,” alisema.

“Yote hayo hayapo, katika kuyaweka kutakuwa na maamuzi ya kuvunja nyumba zilizo mahali hapo.”

Alisema wakati hatua hiyo inatekelezwa, kikubwa ni wale ambao walikuwa wamejenga maeneo yanayotakiwa kwa miradi na hawakujua kwamba ni eneo la barabara au mradi mwingine, wafidiwe.

Butiku alisema inabidi siku zote mambo yanayotendeka yafanyike kwa jina la wananchi kama Rais John Magufuli anavyosema mara kwa mara.

Butiku, ambaye pia ni mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, alitoa mfano wa mpango wa Serikali kupanua barabara ya Morogoro hadi Chalinze, akisema uamuzi huo haukwepeki. “Sijui wanataka kujenga njia saba, kwa sababu magari yameongezeka. Leo kwenda Morogoro inachukua saa tatu mpaka saa nne, zamani ilikuwa ni saa moja na nusu. Hatuwezi kuendelea hivi lazima kupanua ile barabara. Na hivyo zile nyumba zilizopo zitavunjwa,” alisema.

Lakini alisema kuna watu, wakiwamo hata viongozi, hawakujua upana unaotakiwa wa barabara.

“Mara utasikia barabara hizo zilikuwa mita 22 kutoka katikati ya barabara, mara 35 na sasa nasikia mita 120. Hii mia moja na ishirini sijawahi kuisikia,” alisema.

“Mabarabara haya nimeyakuta Uchina huko. Kama ni hivyo, sawa. Lakini inabidi mliowakuta muwalipe fidia.”

Alisema Serikali inabidi iwatendee haki wananchi hao kwa sababu walijua ni upana wa mita 35, leo zimeongezeka hadi mita 120.

“Inawezekana Serikali haina pesa za kutosha, hilo ni tatizo la Serikali, lakini haki ya huyu aliye na nyumba pale inayobomolewa katika eneo ambalo kwa mujibu wa sheria linapanuliwa na hakujua. Hili si jambo la kubishana, ni jambo la haki tu, jamani,” alisema.

“Na haki inazungumzwa. Serikali ina haki ya kusimamia maendeleo na raia wana haki ya kupata haki yao kama katika kupata maendeleo mali zao zinapotea.

“Lakini kusema hamuwezi kubomoa, ohoo ni maskini. Haiwezekani, sasa umaskini tusiwe na barabara?”

Mzee Butiku alisema kwa Taifa lililokomaa kwa miaka mingi, masuala kama hayo yanatakiwa yawe yametungiwa sheria na sheria inayotokana na Katiba ya wananchi.

Hata hivyo, alisema wakati Tanzania inapita kwenye kipindi cha mpito, kuna maeneo mengi ambayo hayajatungiwa sheria na mengine yametungiwa sheria lakini wananchi hawazijui kwa sababu hakuna aliyezieleza kwao.

Alisema kuna sheria zilizotungwa wakati wa uhuru ambazo hata baadhi ya viongozi wa sasa hawazijui.

“Swali, iko sheria, inasemaje? Wananchi wanaifahamu, tusiende ile ya Waingereza kwamba kutojua sheria si kinga ya kuvunja sheria. Hapana, hiyo ipo lakini tuegemee zaidi kwamba watu wetu hawa kwa miaka hii 56 (ya uhuru) sheria hii hawailewi.”

Alihoji, “kwa mfano sheria zetu za ardhi nani anazifahamu, kwa hiyo ni muhimu kuona watu wetu wanaelewa na pale wanapokuwa hawaelewi ni kutoa nafasi kuhakikisha wanazielewa.”

Hata pale zinapotungwa sheria mpya, Butiku alishauri kuhakikisha wananchi wanashirikishwa kupitia wabunge au vyombo vya Serikali ili kuchukua mawazo yao kwa kuwa sheria inayotungwa ni kwa ajili yao.

Jengo la Tanesco

Akizungumzia uamuzi wa kubomoa sehemu yake kupisha upanuzi wa barabara ya Morogoro, Butiku alisema huo ni ujumbe kuwa hakuna nyumba itakayobaki kwenye eneo hilo.

“Juzi nilifurahi Rais Magufuli amezuia bomoabomoa. Nadhani alizuia ili kuondoa wasiwasi, sijui, sitaki kumsemea lakini baadaye akafanya kitu cha mfano akaenda pale Ubungo akasema lile jengo la Tanesco libomolewe,” alisema. “Sasa ukishabomoa jengo la Serikali la nani litabaki? Nadhani hiyo ndiyo meseji. Kama hili limekwenda ili barabara ipite mengine yote yatatoka,” alisema.

Hata hivyo, katika utekelezaji wa uamuzi huo, alisisitiza fidia iwepo.

Mahakama

Akizungumzia wakazi wa Kimara waliokuwa na kesi mahakamani, Mzee Butiku alihoji walikuwa na lengo gani, walipwe fidia au wazuie barabara isijengwe.

Alisema kama ni suala la fidia mahakama inaweza kusema walipwe lakini barabara ijengwe. Kama hakuna pesa kwa sasa, inaweza kusubiri hata ikalipwa mwakani.

No comments:

Post a Comment