Sunday, 26 November 2017

Bondia Ibrahim Class atetea taji La GBC




 BONDIA Mtanzania, Ibrahim Class Mgendera usiku wa kumkia leo amefanikiwa kutetea taji lake GBC uzito wa Light baada ya kumshinda kwa pointi Koos Sibiya wa Afrika Kusini.

Mgendera alishinda kwa pointi za majaji wote, ingawa ushindi wake ulilalamikiwa na mpinzani wake baada ya pambano hilo.

Haukuwa ushindi wa mashaka, kwani Mgendera alipigana vizuri kwa tahadhari kuanzia raundi ya kwanza hadi ya 10 akipiga ngumi za kudonoa kwa wingi katika staili yake ya Orthodox.

Mgendera hakuwa na kazi nyepesi ulingoni, kwani alikutana na bondia mzoefu na mwenye ngumi nzito – lakini akahimili vishindo vyote na kuwafurahisha Watanzania wachache waliojitokeza Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kumshangilia kwa mchezo mzuri.

Dalili za Mgendera kushinda pambano hilo zilianza kuonekana raundi ya nane baada ya kumjeruhi kwenye pua Sibiya ambaye alichafuka damu eneo hilo hadi mdomoni.

Na ni kuanzia raundi hiyo bondia wa Tanzania alianza kutawala pambano baada ya wawili hao kuonekana kupigana sawa katika raundi zilizotangulia. 

Mgendera aliyezaliwa Oktoba 10, mwaka 1990 eneo la Ipogolo, wilayani Mufundi mkoani Iringa, alitwaa taji hilo Julai 1, mwaka huu baada ya kumpiga Jose Luis Forero Atencio wa Panama kwa pointi Jijini Berlin, Ujerumani. 

Hilo linakuwa pambano la 21 Mgendera kushinda kati ya 25 aliyocheza, akiwa amepoteza mapambano manne.

No comments:

Post a Comment