Tuesday 31 October 2017

Yanga kumaliza hasira zao kwa Singida United.

KOCHA WA TIMU HIYO, GEORGE LWANDAMINA.

BAADA ya kuambulia pointi moja dhidi ya Simba kwenye mechi iliyopita katika Uwanja wa Uhuru, Yanga itaondoka Dar es Salaam kesho kuelekea Singida ikiwa na hasira ya kukisambaratisha kikosi cha Hans van der Pluijm, Singida United.

Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, kama ilivyo kwa Singida United na Simba, Jumamosi ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya watani zao hao wa jadi kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara.

Kikosi hicho cha Yanga katika safari hiyo, kitaendelea kuikosa huduma ya wachezaji wake wa kigeni, Amissi Tambwe, Donald Ngoma na Thabani Kamusoko ambao bado hawajapona kwa asilimia 100.

Akizungumza na Nipashe jana, kocha wa timu hiyo, George Lwandamina, alisema kuwa matokeo waliyoyapata dhidi ya Simba yamewapa ari ya kufanya vizuri kwenye mchezo wao huo wa ugenini.

"Hatutakuwa na Tambwe, Ngoma na Kamusoko kama ilivyokuwa kwenye mchezo dhidi ya Simba, lakini hilo halinipi shida sana, nakiamini kikosi changu," alisema Lwandamina.

Alisema tofauti kwao ni kwa kuwa wanacheza mchezo huo ugenini na Singida ni moja ya timu imara kwenye Ligi Kuu msimu huu.

"Naamini tutafanya vizuri, wachezaji wangu wana ari na morali ya juu hasa baada ya matokeo tuliyoyapata dhidi ya Simba... tumekuwa na wachezaji majeruhi ambao ni muhimu na mchango wao unahitajika, lakini tumefanikiwa kuhimili changamoto za Ligi Kuu," alisema kocha huyo raia wa Zambia.

Kikosi cha timu hiyo leo kitaanza mazoezi ya uwanjani kwenye uwanja wa Uhuru baada ya jana kufanya mazoezi ya viungo gym.
Yanga wataondoka Dar es Salaam leo kwa basi kuelekea Singida tayari kwa mchezo huo utakaopigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Namfua ambao ukarabati wake umekamilika.

Mabingwa hao watetezi wanashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi wakiwa na pointi 16 sawa na vinara Simba, Mtibwa Sugar na Azam FC, lakini Wanamsimbazi hao wanabebwa na tofauti nzuri ya mabao ya kufunga na kufungwa

No comments:

Post a Comment