Thursday, 2 November 2017

Omog hafukuzwi ng’o: Simba



KAIMU RAIS WA KLABU HIYO, SALIM ABDALLAH "TRY AGAIN.

WAKATI mkataba wa Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog, ukiwa umebakiza miezi minne kumalizika na hakuna mazungumzo yoyote ya kusaini mkataba mpya yaliyofanyika, Kaimu Rais wa klabu hiyo, Salim Abdallah "Try Again", ameibuka na kusema kuwa kocha huyo hafukuzwi.

Minong'ono ya kutimuliwa kwa Omog imeendelea kwa kasi baada ya kutua kwa Mrundi Masoud Djuma Irambona, ambaye amerithi mikoba ya Jackson Mayanja aliyeamua kuachia ngazi na kurejea kwao Uganda kumaliza matatizo ya kifamilia.

Akizungumza na Nipashe jana, Salim, alisema kuwa Omog bado ni kocha wa Simba na hakuna kikao chochote ambacho kimefanyika na kufikia uamuzi wa kumtimua kocha huyo raia wa Cameroon.

Salim alisema kuwa mpaka sasa timu yao haijapoteza mchezo wowote kwenye ligi na anawaomba wote ambao wanafikiria Omog ataondoka kwenye klabu hiyo inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, kwa sasa waache kuwaombea "mabaya".

"Kuna watu wana ndoto na matarajio ambayo hatuwezi kuwazuia kuyafikiria, hatujafungwa, tunaongoza ligi, ligi ni ngumu msimu huu, sio ya kawaida, timu nne zote zinalingana pointi, haijawahi kutokea," alisema Salim ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kundi la Friend's of Simba.

Hata hivyo, Salim alikataa kuweka wazi kama klabu ina mpango wa kumpa mkataba mpya Omog ambaye aliwahi kuifundisha Azam FC, lakini akikiri kuwa waliwahi kufanya mazungumzo na Kocha Mkuu wa Lipuli FC, Selemani Matola ili kuchukua nafasi ya Mayanja.

"Mkataba ni siri kati ya sisi na kocha, hatuwezi kuweka hadharani, ila tuna mkataba naye mrefu, hatuna mpango wa kumfukuza, pia siwezi kusema kesho kitatokea nini, anaweza yeye akaamua kuachana na sisi na kwenda mahali kwingine," alisema Salim.

Kiongozi huyo aliongeza kuwa Omog na msaidizi wake wanafanya kazi kwa ushirikiano na tayari wameshaanza kutoa mapendekezo ya kuimarisha kikosi cha timu hiyo kuelekea dirisha dogo la usajili.

"Omog ametupa ubingwa wa FA, tukamaliza katika nafasi ya pili msimu uliopita, kwa sasa Simba iko vizuri, hakuna migogoro na viongozi tunajenga mifumo imara na sahihi, tunataka kuiendesha klabu kisasa, tunaachana na kufanya mambo kwa mazoea," aliongeza kiongozi huyo.

Kikosi cha Simba kinatarajia kuondoka jijini kesho kuelekea Mbeya kwa ajili ya kuwafuata wenyeji wao Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kupigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Sokoine jijini humo

No comments:

Post a Comment