SWEDEN imetoa Sh. bilioni 80.4 kwa Umoja wa Mataifa (UN) ili kusaidia kuzuia vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto na kuhamasisha wanawake kushiriki katika siasa nchini.
Fedha hizo pia zitaelekezwa katika kusaidia kukuza uchumi, upatikanaji wa ajira, kuimarisha utawala bora na usawa wa kijinsia.
Katika hafla ya kutiliana saini jijini Dar es Salaam jana, Balozi wa Sweden nchini, Katarina Rangnitt, alisema msaada huo kwa kiasi kikubwa utaelekezwa kusaidia masuala ya kimaendeleo kwenye maeneo yanayomgusa mwanamke.
Alisema Sh. bilioni 33 zitatumika kuwasaidia wafanyabiashara wadogo ili kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira hususani kwa wanawake na vijana wakati Sh. bilioni 22 zitatumika kwa ajili ya kuleta uwazi na uwajibikaji serikalini, kuimalisha shughuli za kibunge, haki za binadamu, kuwakinga waandishi wa habari na kuziinua redio ndogo zisizosikika ili wananchi wapate zaidi habari.
Alisema Sh. bilioni 26.4 zitatumika kuwahamasisha wanawake kushiriki siasa na kuzuia vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Balozi huyo alisema msaada huo pia utakuza uchumi na kusaidia wananchi na nchi kufikia malengo yake ya kuwa nchi ya uchumi wa kati.
"Kupitia Umoja wa Mataifa tunaiunga mkono Tanzania katika kufikia malengo iliyojiwekea. Pia tunatambua mchango wa Umoja wa Mataifa katika kufanikisha maendeleo endelevu,” alisema Rangnitt.
Katika hafla hiyo, Mratibu Mkaazi wa UN nchini, Alvaro Rodrigues, alisema Sweden imekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya Tanzania kwa miongo mingi kwa kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum.
Alisema msaada huo utaisaidia UN kuwafikia watu wasio na ajira, kuwawezesha wanawake pamoja na kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto
No comments:
Post a Comment