Friday 3 November 2017

Mashabiki waYanga watolewa hofu

KOCHA WA YANGA, GEORGE LWANDAMINA.

LICHA ya kuwakosa nyota wake wanne, kocha wa Yanga, George Lwandamina, amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo kwa kuwa timu yake inauwezo wa kupata matokeo mazuri kwenye mchezo wa kesho dhidi ya Singida United.

Yanga ipo Singida bila ya washambuliaji wake, Donald Ngoma na Amisi Tambwe pamoja na Thaban Kamusoko na Juma Abdul.
Wakati Ngoma, Tambwe na Kamusoko wakiukosa mchezo huo kutokana na kuwa majeruhi, Abdul anakabiliwa na kadi tatu za njano zinazomfanya kukosa mchezo huo.

Akizungumza na gazeti hili muda mfupi kabla ya kuanza safari ya kuelekea Singida, Lwandamina, alisema kuwa anaamini wachezaji wake ambao wapo ndani ya kikosi kilichoelekea Singida wanauwezo mkubwa wa kuwakabili wenyeji wao.

"Nina imani na wachezaji wangu wote, tunaenda kukabiliana na Singida United huku nikiamini tunauwezo wa kupata ushindi," alisema Lwandamina.

Alisema wamejitahidi kufanya marekebisho kwenye makosa madogo madogo aliyoyaona kwenye mchezo uliopita.

"Tumefanyia kazi suala la umaliziaji, yapo makosa madogomadogo ambayo niliyaona kwenye mchezo dhidi ya Simba, nataka
tutumie vizuri nafasi tunazozitengeneza ndani ya uwanja," aliongezea kusema Lwandamina.

Cannavaro: Hautakuwa mchezo rahisi

Nahodha wa timu hiyo, Nadir Haroub 'Cannavaro', aliiambia Nipashe kuwa mchezo huo wa kesho hautakuwa rahisi kutokana na ubora wa kikosi cha wapinzani wao.

Alisema Singida United wamefanya usajili mzuri na wanachezaji wenye uzoefu na ligi hivyo wao (Yanga) watacheza kwa tahadhari kuhakikisha wanapata ushindi.

“Singida si timu ya kubeza… tutapambana kuhakikisha tunapata ushindi," alisema Cannavaro.
Mchezo huo wa kesho utachezwa kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida

No comments:

Post a Comment