Thursday, 2 November 2017

Viongozi wawili wa Acacia wajiuzulu



Dar es Salaam. Wakati utekelezaji wa makubalino baina ya Serikali na Barrick ukisubiriwa, Ofisa Mtendaji Mkuu na Ofisa Mkuu wa Fedha wa Kampuni ya Acacia, wametangaza kujiuzulu kuanzia leo Alhamisi.

Kwenye barua yake, Ofisa Mtendaji Mkuu, Brad Gordon amesema anataka kurudi nyumbani Australia kusimamia masuala ya familia yake wakati Ofisa Mkuu wa Fedha, Andrew Wray akisema amepata fursa nzuri zaidi sehemu nyingine.

“Pamoja na uamuzi huo, wote wataendelea kuhudumu kwenye nafasi hizo wakati wakikabidhi majukumu ya ofisi kwa warithi wao,” imesema taarifa ya Acacia iliyotolewa leo Alhamisi asubuhi.

Kuziba nafasi hizo, Bodi ya Wakurugenzi wa Acacia imemtangaza Peter Geleta kuchukua majukumu ya ofisa mtendaji mkuu baada ya Gordon na Jaco Maritz kusimamia masuala yote ya fedha za kampuni hiyo.

Wote wawili walikuwa watendaji wa Acacia kwa muda mrefu. Geleta alikuwa mkuu wa oganaizesheni wakati Maritz alikuwa meneja mkuu wa idara ya fedha.

“Licha ya majukumu ya uendeshaji, Geleta atahudhuria vikao vya bodi vitakavyofanyika mwishoni mwa mwaka huu badala ya Gordon na kuifanya idadi ya wajumbe kuendele akubaki saba,” imesema taarifa hiyo.

No comments:

Post a Comment