Tuesday, 31 October 2017

Polisi wakamata Vifaranga vya kuku 6,400



Arusha. Vifaranga vya kuku 6,400 vinatarajiwa kuchomwa moto baada ya kunaswa vikiingizwa nchini kupitia Longido mkoani Arusha.

Vifaranga hivyo vilikamatwa juzi vikitokea nchini Kenya.

Taarifa zinasema thamani ya vifaranga hivyo ni Sh12.5 milioni na ni mali ya mfanyabiashara Mary Matia (23) mkazi wa Mianzini jijini Arusha anayeshikiliwa na polisi.

Akizungumza na Mwananchi katika mpaka wa Kenya na Tanzania eneo la Namanga, ofisa mfawidhi wa Kituo cha Udhibiti wa Magonjwa ya Mifugo Kanda ya Kaskazini, Obedi Nyasembwa alisema tangu mwaka 2007 Serikali ilipiga marufuku kuingiza mayai na vifaranga kutoka nje ya nchi.

Alisema uamuzi huo wa Serikali ulichukuliwa ili kudhibiti magonjwa ya mifugo ukiwamo wa mafua ya ndege.

“Kwa mujibu wa Sheria ya Magonjwa ya Wanyama ya mwaka 2003, vifaranga hivi tutaviteketeza kwa kuwa vinaweza kuwa na magonjwa,” alisema.

Meneja Msaidizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika mpaka wa Namanga, Edwin Iwato alisema kwa mujibu wa sheria vifaranga hivyo havikupaswa kuingizwa nchini, hivyo licha ya kuviteketeza, gari lililotumika kuvisafirisha litatozwa faini.

Akizungumza akiwa chini ya ulinzi wa polisi, mfanyabiashara Matia alikiri kuingiza nchini vifaranga hivyo akisema hakuwa akijua kama uingizaji umepigwa marufuku.

“Naomba wasivichome moto vifaranga, ni bora waniruhusu nivirudishe Kenya kwa kuwa ninadaiwa Sh12.5 milioni nilikovinunua,” alisema.

Hata hivyo, ofisa mfawidhi mkaguzi wa Mifugo, Medard Tarimo alisema kwa muda mrefu yamekuwapo malalamiko ya kuingizwa nchini vifaranga na mayai lakini wamekuwa wakishindwa kuwakamata wahusika.

“Wamekuwa wakipita njia za panya usiku na kuingiza nchini jambo ambalo ni la hatari kwa afya za binadamu kwa kuwa nchi jirani tu ya Uganda kuna ugonjwa wa mafua ya ndege,” alisema

No comments:

Post a Comment