Tuesday 28 November 2017

Magunia 150 ya majani ya chai yateketeza



MAJANI ya chai magunia 150 ambayo hayafai kwa matumizi ya binadamu yaliyoingizwa nchini kwa njia za panya kupitia mipaka ya Holili na Tarakea, Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro yameteketezwa kwa moto kuepusha kusambazwa kwa walaji.

Uteketezaji wa chai hiyo uliratibiwa na kutekelezwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Taarifa zilizoifikia Nipashe na kuthibitishwa na Mkaguzi wa TFDA, Edward Mamlawa, zimeeleza kuwa utafiti uliofanywa na wataalamu wa vyakula ulibaini kwamba majani hayo hayafai kwa matumizi ya binadamu.

“Ni kweli tumeyateketeza majani ya chai yenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 10, kwa sababu kama yangeingia sokoni yangeleta madhara makubwa kwa afya za binadamu. Tumeifanya kazi hiyo kwa ushirikiano na TRA,” alisema Mamlawa.

Wilaya ya Rombo, ina njia za panya zaidi ya 360 zilizopo kwenye mipaka ya Holili na Tarakea inayozitenganisha nchi za Tanzania na Kenya.

Kutokana na hasara iliyopatikana kuteketezwa kwa bidhaa hizo, Mkaguzi huyo alishauri   wafanyabiashara wafuate sheria za uingizwaji wa bidhaa za chakula nchini ili kuepuka hasara na kulinda afya za walaji.

Meneja wa TRA, Mkoa wa Kilimanjaro, Msafiri Mbibo, aliwataka wafanyabiashara na walipa kodi kuacha kutumia njia za magendo kuvusha bidhaa kutoka nje ya nchini na badala yake watumie njia halali na kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo ya taifa.

Meneja Msaidizi anayeshughulikia Idara ya forodha mkoani Kilimanjaro, Godfrey Kitundu, akizungumzia bidhaa hizo alisema biashara kati ya nchini ya Kenya na Tanzania ni nzuri na kwamba changamoto kubwa ni uwepo wa njia za panya ambazo zinatumiwa na wafanyabiashara wasio waadilifu kuingiza bidhaa mbalimbali ambazo hazijafanyiwa ukaguzi.

No comments:

Post a Comment