Wednesday, 24 January 2018

Rais wa TFF aguswa na msiba wa Kocha wa Mwadui


Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Wallace Karia ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu Jumanne Ntambi na wachezaji wa Mwadui kwa kuondokewa na kocha wao usiku wa kuamkia leo huku akiwataka wafiwa wawe na moyo wa subira

Rais Karia amesema hayo katika salamu zake zilizotolewa rasmi na Shirikisho hilo huku akisema ameshtushwa kupata taarifa hizo kwani marehemu Ntambi alikuwa na mchango mkubwa katika soka la Tanzania.

"Kifo cha Kocha Ntambi kimenishtua sana na kwa niaba ya Shirikisho natoa pole kwa wafiwa, nawaomba wawe na subira katika kipindi hiki kigumu kwao kumpoteza mpendwa wao. Hakika alikuwa kocha aliyejitahidi kuibua vipaji na amekuwa na mchango mkubwa katika mpira wa miguu ambao bado alikuwa anautumikia mpaka kifo chake," alisema Rais Karia.

Enzi za uhai wake Jumanne Ntambi aliwahi kufundisha timu za Kahama United ya Shinyanga, Mlale JKT ya Ruvuma, Panone ya Kilimanjaro, timu ya mkoa wa Shinyanga Igembe Nsabo na mpaka mauti yanamkuta alikuwa akiifundisha Mwadui ya Shinyanga akiwa kocha msaidizi.

No comments:

Post a Comment