Wimbi la madiwani wa Chadema kujivua uanachama na kujiunga na CCM limezidi kukikumba chama hicho kikuu cha upinzani nchini baada ya leo Januari 27, mwaka 2018 madiwani wake wanne kujiunga na chama tawala, wakiwemo watatu wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo mkoa wa Kilimanjaro.
Wakati diwani wa Kimara (Chadema), Pachal Manota akitambulishwa katika uzinduzi wa kampeni za ubunge za chama hicho jimbo la Kinondoni zilizofanyika viwanja wa Biafra, wenzake watatu walitambulishwa kwenye mkutano wa kampeni za ubunge jimbo la Siha mkoani Kilimanjaro uliofanyika eneo la Makiwaru.
Madiwani hao ni Juliana Malamsha, Martha Ushaki (wote Viti maalum) na Frank Umega (kata ya Kelamfua).
Wametambulishwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM-Bara, Rodrick Mpogolo wakati akimnadi mgombea ubunge wa chama hicho jimbo la Siha, Dk Godwin Mollel.
Mpogolo amesema viongozi wa upinzani wanajiunga na CCM baada ya kubaini ajenda ya kuwahudumia wananchi, kuwaletea maendeleo ipo katika chama tawala pekee .
"Kuna wimbi kubwa la viongozi wa upinzani kujiunga na CCM. Hii inatokana na viongozi hao kubaini kuwa ajenda ya huduma na maendeleo iko katika chama hiki pekee. Tupeni Dk Mollel ili tuweze kutekeleza agenda hii muhimu,” amesema Mpogolo.
Uamuzi wa madiwani wa Chadema kuhamia CCM mpaka sasa umeziweka Halmashauri tano zilizo chini ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuwa hatarini kuchukuliwa na CCM.
Halmashauri hizo ni Arusha, Arumeru, Hai, Siha na Iringa ambazo madiwani wake, hasa kutoka Chadema wametimkia CCM kutokana na sababu tofauti, kubwa ikiwa ni kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais John Magufuli.
No comments:
Post a Comment