Thursday, 25 January 2018

Stand United yatamba kuiburuza Ndanda leo



 Stand United inaikaribisha Ndanda leo Alhamisi katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaofanyika kwenye Uwanja wa Kambarage Shinyanga.

 Kivutio katika mchezo huo kitakuwa ni nahodha  wa Ndanda, Jacob Massawe kurejea katika uwanja huo kuikabili  timu yake ya zamani Stand United.

Kocha msaidizi wa Stand United, Athuman Bilal 'Bilo' amesema wako vizuri kuhakikisha wanaondoka na pointi zote tatu kwenye uwanja wao wa nyumbani.

Hata hivyo Bilo alisema itakuwa mechi ngumu kwani zinakutana timu zenye pointi sawa hivyo kila mmoja atataka ushindi ili kujiweka vizuri kwenye msimamo wa ligi.

"Tumefanya maandalizi yetu vizuri na tuko tayari kwa mchezo kuhakikisha tunavuna pointi zote tatu.

"Itakuwa mechi ngumu kwani Ndanda ina wachezaji wazuri na pia kama unavyojua wote tuna pointi sawa hivyo itakuwa ni vita ya kuwania ushindi" alisema Bilo.

Naye kocha wa Ndanda, Malale Hamsini alisema anajua ugumu wa kucheza ugenini lakini watapambana ili kuweza kupata ushindi.

"Hii ni mechi ya pili Kanda ya ziwa baada ya ile ya Mwadui kutoka sare wiki iliyopita sasa tunahitaji ushindi dhidi ya Stand United ili kujiweka vizuri kwenye msimamo wa ligi," alisema Malale.

No comments:

Post a Comment