Friday, 26 January 2018

Kesi ya Tido Mhando yaahirishwa hadi Februari 23


Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando amepata dhamana baada ya kukidhi masharti na kutakiwa kurejea Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Februari 23, mwaka huu.

Tido alifikishwa mahakamani hapo saa 5:22  asubuhi na aliingizwa katika ukumbi wa mahakama ya wazi kabla ya kusomewa mashtaka matano.

Leo Januari 26, mwaka 2018 wakili wa Takukuru, Leonard Swai amedai mbele ya hakimu mkazi mkuu wa makahama hiyo,  Victoria Nongwa kuwa Mhando anatuhumiwa kwa mashtaka matano.
Swai amesema Juni 16, 2008 katika maeneo ya Dubai, United Arab Emirates (UAE), Tido akiwa mwajiriwa wa TBC kama Mkurugenzi Mkuu kwa makusudi alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mkataba wa makubaliano kwa ajili ya kuendesha na utangazaji wa vipindi vya televisheni kati ya TBC na Channel 2 group Corporation ( BV1) bila ya kupitisha zabuni kinyume  na sheria ya manunuzi na kuisababishia BVl kupata manufaa.

Shtaka la pili, Tido anadaiwa Juni 20, 2008  katika maeneo ya utekelezaji wa kazi yake alitumia madaraka vibaya kwa kusaini makubaliano (wakuu wa makubaliano) kwa utangazaji wa digital duniani kati ya TBC na BVl.

Shtaka la tatu, Agosti 11, 2008  na Septemba 2008 katika maeneo hayo, Tido anadaiwa kutumia  vibaya madaraka yake kwa kusaini mkataba wa makubaliano (kuongeza wakuu wa mkataba ) kwa ununuzi, usambazaji kufunga vifaa vya usambazaji na mnara wa utangazaji kati ya TBC na BVI na kuisababishia BVI kupata faida.

Shtaka la nne, Tido anadaiwa Novemba 16,2008 akiwa Dubai, United Arab Emirates alitumia vibaya madaraka yake kwa kusini mkataba wa makubaliano (kuongeza wakuu wa mkataba ) kwa kuendesha miundombinu ya utangazaji (DTT broadcast infrastructure) kati ya TBC na BVI na kusababisha BVI kupata manufaa.

Katika shtaka la tano, Tido anadaiwa kati ya Juni 16 na Novemba 16, 2008 katika maeneo hayo ya United Arab Emirates aliisababishia hasara TBC ya Sh 887, 122,219.19.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Tido ambaye anatetewa na wakili Ramadhani Maleta alikana mashtaka yote.

Swai alidai mahakamani hapo kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.
Hakimu Nongwa alimtaka mshtakiwa kutoa fedha taslimu mahakamani hapo Sh444 milioni ama hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha.

Mbali na sharti hilo, pia awe na wadhamini wawili ambapo watasaini hati ya dhamana ya maneno yenye thamani ya Sh500 milioni na asitoke nje ya nchi bila ya kuwa na kibali cha mahakama.
Mshtakiwa alikamilisha masharti hayo kwa kuwasilisha hati za mali na wadhamini wawili nyakati za saa sita mchana na kuondoka.

Kesi imeahirishwa hadi Februari 23, 2018 kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali (PH).
Kuhusu dhamana hiyo, DPP alipeleka hati ambayo inaipa mamlaka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuisikiliza kesi hiyo.

Mhando ni miongoni mwa waandishi wa habari na watangazaji mahiri na wakongwe ndani na nje ya nchi ambaye amewahi kufanya kazi Shirika la Utangazaji Uingereza (BBC).
Pia amewahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) inayochapisha magazeti ya Mwananchi, Mwanspoti na The Citizen na sasa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Azam Media.

No comments:

Post a Comment