
WATU 15 kati ya 20 wanaokwenda kwa uchunguzi katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), sawa na asilimia 75, wanakutwa na maradhi mbalimbali ya moyo, imefahamika.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Magonjwa ya Moyo katika taasisi hiyo, Dk. Peter Kisenge, mbali na watu hao, alisema asilimia mbili hadi tatu ya watoto wanaozaliwa nchini wana tatizo la moyo.
Kutokana na takwimu hizo, alisema ni vyema Watanzania wakafika katika taasisi hiyo kubwa Afrika Mashariki na Kati kwa ajili ya uchunguzi, ikiwa ni pamoja na kujiunga na bima ya afya kwa kuwa huduma za matibabu ni kubwa.
Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo, alisema JKCI kwa kushirikiana na taasisi za Israel na Ujerumani, wameokoa Sh. milioni 800 ambazo zingetumika kuwapeleka nje ya nchi watoto 30 kwa matibabu ya moyo.
Taasisi hizo ni Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto ya Israel na Kituo cha Moyo cha Berlin, Ujerumani, ambao hadi sasa wamewafanyia upasuaji wa bila kufungua kifua watoto 15.
“Upasuaji unatumia mtambo wa Cathlab umefanyika katika kambi maalumu iliyoanza Januari 20, mwaka huu na itamalizika kesho (leo). Matibabu yaliyofanyika ni kuzibua matundu kwenye moyo na kutanua mishipa ya moyo kwa watoto wenye umri wa kuanzia mwezi mmoja hadi miaka 18,” alisema.
Kwa mujibu wa Kisenge, kambi hiyo ilikwenda sambamba na uchunguzi wa moyo kwa watoto 32 ambao kati yao 20 watafanyiwa matibabu katika kambi hiyo na wengine 12 watatibiwa na madaktari hapa nchini kuanzia wiki ijayo.
“Tumepanga kufanya matibabu kwa watoto 20, tunaamini hadi kambi itakapomalizika watakuwa wamepata matibabu. Watoto 15 waliopata matibabu wamesharuhusiwa na waliobaki wanaendelea vizuri,” alisema.
“Tumetoa elimu ya upasuaji wa moyo wa bila kufungua kifua kwa watoto, jinsi ya kuwahudumia waliofanyiwa upasuaji. Waliopata mafunzo ni madaktari, wauguzi, wataalamu wa kutoa dawa za usingizi na wataalamu wengine wa chumba cha upasuaji,” alifafanua.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, asilimia 90 ya matibabu bila kufungua kifua yanafanywa na madaktari wa Tanzania kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo, Naiz Majani, alisema wanawake wanapaswa kufanya uchunguzi wakiwa na mimba ya miezi minne, ili watakapojulikana na tatizo wajifungue katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, hivyo kuwa rahisi kupata matibabu.
Alisema kuna wanawake 35 wenye tatizo la moyo, kati yao watano wamejifungua mmoja mwanawe alifariki dunia kwa ugonjwa mwingine, wawili wana matundu makubwa kwenye moyo na mmoja limeanza kupungua.
“Tunawashauri wazazi na walezi wasisahau kupima afya zao watoto wao watakapoona kuna hali ya tofauti katika ukuaji wa mtoto kwani magonjwa mengi yanaanzia utotoni,” alisema.
Kwa mujibu wa Dk. Majani, mtoto akianza kuugua magonjwa ya moyo, wazazi wengi wanadhani ni matatizo ya kifua, lakini baada ya kuwafikisha hospitalini na kufanyiwa vipimo ndipo inagundulika.
Tangu mwaka 2015 hadi sasa, watoto 46 wamefanyiwa upasuaji wa moyo nchini Israel na kwamba gharama zimekuwa zikitolewa na taasisi za Israel na Ujerumani kwa makubaliano ya kirafiki na JKCI.
Watoto 79 walitibiwa kwenye kambi maalumu kuanzia mwaka 2015 hadi 2017 na kwamba huduma hizo ni bure kwa watoto wenye matatizo hayo.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), watu milioni moja wanakadiriwa kuwa na tatizo la moyo.
No comments:
Post a Comment