Friday, 26 January 2018

Hospitali ya Bugando yanufaika na mashine za CT-SCAN


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amezindua huduma za mashine ya CT – SCAN katika hospitali ya Rufaa ya kanda ya Ziwa Bugando jijini Mwanza,ambazo zilisimama kwa muda wa miaka minne iliyopita, baada ya mashine iliyokuwepo awali kuharibika mwaka 2014.

Mashine hiyo ya kisasa,iliyonunuliwa nchini Ujerumani kwa gharama ya shilingi Bilioni 1.7,imesimikwa na kufanyiwa majaribio na uhakiki kutoka tume ya mionzi Tanzania na kuthibitika kuwa na uwezo wa kufanya kazi ipasavyo.Mashine hiyo kwa mujibu wa daktari bingwa wa mionzi Dk.Godfrey Kasanga itakuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa 100 kwa siku.

Askofu wa jimbo katoliki la Geita,Mhashamu baba askofu Flavian Kasala,ambaye amemwakilisha Mwenyekiti wa bodi ya uendeshaji ya hospitali hiyo,Mhashamu Askofu Mkuu jimbo kuu la Mwanza Yuda Thadei Rwaichi,amewataka watumishi wa kitengo kitakachosimamia huduma za mashine hiyo kuitunza na kuacha kuihujumu.

Kwa upande wake,Mkurugenzi mkuu wa hospitali ya rufaa ya Kanda ya ziwa Bugando Dk.Abel Makubi ameiomba serikali kuanzisha taasisi ya moyo katika hospitali hiyo ili kupunguza idadi ya wagonjwa kutoka mikoa ya kanda ya ziwa wanaokwenda Dar es Salaam kutafuta matibabu ya moyo katika Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete.


No comments:

Post a Comment