Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira imeiagiza Serikali kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki kutoka nje ya nchi ili kulinusuru Taifa na madhara yanayotokana na mifuko hiyo.
Maagizo hayo yalitolewa baada ya kamati hiyo jana kukutana na Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Akizungumza jana, mwenyekiti wa kamati hiyo, Sadiq Murad alisema walipata maelezo kutoka serikalini kuwa uzalishaji katika viwanda 41 vya plastiki nchini ulikuwa ni tani 73 katika mwaka 2016.
Hata hivyo, alisema mifuko iliyoingia nchini kupitia bandarini na mipakani ilikuwa tani 1,375.
“Kamati ilishauri ipigwe marufuku mifuko ya plastiki kutoka nje ya nchi na iwekwe tahadhari katika mipaka yetu,” alisema.
Alisema kamati inaitaka Serikali kufanya uhakiki wa uzalishaji katika viwanda vya nchini ambavyo vimepunguza uzalishaji ili waweze kukaa chini na kuzalisha mifuko ambayo itakayokidhi mahitaji na vigezo.
“Na hii itakuwa ni ya muda kuzalisha mifuko hiyo kwa masharti ya vigezo baadaye Tanzania isiwe na uzalishaji wa mifuko hii tena inayoharibu mazingira,” alisema.
Murad alisema zipo nchi nyingine kama Kenya, Rwanda, Uganda na Zanzibar ambazo zimepiga marufuku uzalishaji na uingizaji wa mifuko hiyo na kutafuta mifuko mingine inayotengenezwa na nguo, karatasi na majani.
Alisema mfano mzuri ni Zanzibar ambayo imepiga marufuku mifuko hiyo tangu mwaka 2016 na mtu anapoingia na mifuko hiyo bandarini hunyang’anywa na kupewa mingine.
“Tueleweke kabisa sisi kama kamati hatutaki kiwanda chochote kifungwe, tunataka uzalishaji kwa kufuata masharti na vigezo. Tunaunga mkono juhudi za Rais John Magufuli za kuipeleka nchi katika uchumi wa viwanda lakini vigezo na masharti lazima yazingatiwe,” alisema.
Akizungumzia agizo hilo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba alisema hawaja japelekewa rasmi hayo mapendekezo. Hata hivyo alisema watapiga marufuku mifuko yote ya ndani na nje. “Wenye viwanda wajiandae maana yake dhamira ya Serikali wanaijua tangu mwaka 2016,” alisema
No comments:
Post a Comment