Wasomi wameifananisha na rushwa ya uchaguzi ahadi iliyotolewa kwa wananchi wa Jimbo la Siha kuwa watapata neema iwapo watamchagua mgombea wa CCM, Dk Godwin Mollel ambaye anatetea ubunge aliouachia mwishoni mwa mwaka jana kwa kujivua uanachama wa Chadema.
Ahadi hiyo ilitolewa juzi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo wakati akimnadi mgombea Dk Mollel.
Wamesema kauli hiyo inaweza kusababisha ushindi wa Dk Mollel kupingwa, huku Profesa Abdallah Safari akienda mbali zaidi na kufananisha kauli hiyo na iliyowahi kutolewa na mawaziri kadhaa wakati wa uchaguzi mdogo wa ubunge Igunga mwaka 2011 na kusababisha ushindi wa aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk Dalali Kafumu kubatilishwa na Mahakama.
Akiwa jukwaani, Jafo alisema CCM ndicho chama chenye Serikali na ndicho kinachoweza kutatua changamoto na shida za wananchi, na kwamba akishinda Serikali itafanya kila njia kuboresha maisha ya wananchi.
Jafo alisema ikiwa wananchi watamchagua Dk Mollel ambaye hivi karibuni alijiondoa Chadema na kugombea tena nafasi hiyo kupitia chama tawala, Serikali itashirikiana naye na miaka miwili iliyobaki Siha itakuwa moja ya wilaya ambazo zitapiga hatua kubwa na kufanya vizuri katika utekelezaji wa maendeleo.
Lakini ahadi hiyo ya Waziri Jafo kwa wananchi wa Siha haijapokelewa vizuri na wasomi waliohojiwa na Mwananchi.
“It is a sort of (ni kama-rushwa) kwa wapiga kura kupitia miradi ya maendeleo ya Serikali, anaposema Dk Mollel akishinda ndipo hospitali ijengwe,” alisema Dk Hamad Salim, mhadhiri wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
Dk Salim alisema kauli hiyo inaashiria rushwa na kushauri mawaziri watenganishwe na vyama vya siasa.
“Kuna haja ya kutenganisha mawaziri na vyama vya siasa. Mawaziri wanapaswa kuwa watendaji wa Serikali. Kauli ile inakera mno. Ni afadhali tu angesalimia na kuongea kama mwana CCM kuliko kuihusisha Serikali,” alisema.
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda alisema kauli ya Jafo inakwenda kinyume na sheria ya gharama za uchaguzi.
“Sheria ya gharama za uchaguzi iliyoanzishwa mwaka 2010 haikusikika sana kwenye uchaguzi wa 2015, lakini inaeleza vizuri. Kifungu cha 21(a) na (c) vinakatza hata mgombea tu kuahidi kutoa zawadi ili achaguliwe, kwa sababu itahesabika kama rushwa?” alisema Dk Mbunda.
Naye Profesa Safari alisema ikiwa mgombea wa Chadema katika jimbo hilo, Elvis Mosi atashindwa katika uchaguzi huo, wataitumia kauli ya Jafo kupinga matokeo mahakamani.
Katika ufafanuzi wake, Profesa Safari alisema kauli ya Jafo inaashiria utoaji wa rushwa na inaweza kusabababisha kesi kama ya Jimbo la Igunga.
“Hiyo ni corruption (rushwa) kabisa na ndiyo maana ile kesi ya Igunga tulishinda,” alisema Profesa Safari ambaye ni makamu mwenyekiti wa Chadema-Bara.
“Ni kauli mbaya sana na inaweka mazingira ya kupinga uchaguzi huo endapo mgombea wa CCM atashinda. Kesi ya Igunga imekuwa ikirejewa katika kesi nyingi tu.”
Hata hivyo, mkurugenzi wa taasisi ya Fordia, Buberwa Kaiza amesema kauli ya Jafo inaweza isihesabike kama rushwa kwa sababu hospitali yenyewe haijajengwa, japo kimaadili kutoa ahadi kama hiyo ni kosa.
“Maadili ya uchaguzi yanazuia kabisa mtu kutumia mali za Serikali kufanyia kampeni chama cha siasa. Maadili pia yanazuia kabla na baada ya uchaguzi kutumia majukumu ya Serikali kama ahadi ya uchaguzi,” alisema.
“Kama ilani ya uchaguzi ya CCM ilisema watajenga hospitali na yeye alikuwa akikumbushia, sawa. Lakini kama alisema mgombea wao akichaguliwa ndipo watajenga, hilo ni kosa.”
No comments:
Post a Comment