Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amezindua jengo la upasuaji katika Hospitali ya Mwananyamala lililojengwa kwa msaada wa kampuni ya GSM.
Katika uzinduzi huo Makonda amesema kuwa Serikali itaandaa mpango wa kuwezesha wananchi kupata matibabu kwa kutumia kadi ya bima ya afya katika hospitali zote za umma.
Aidha amesema mwananchi mkoani Dar es Salaam ambaye hatakuwa na kadi hiyo hataweza kupata huduma.
Amesema lengo la mpango huo ni kuwawezesha wananchi kuwa na uhakika wa matibabu hata wakati hawana fedha.
"Ni muhimu tuingie kwenye mfumo wa matibabu kwa kadi badala ya kuchangishana na kusumbua watu kwenye simu. Itafikia wakati mtu ambaye hana kadi hatatibiwa kwenye hospitali zetu," amesema.
Serikali inaendelea kuboresha mazingira na miundombinu ili kuwapatia wananchi huduma bora ya afya.
Makonda aliyefanikisha ujenzi wa jengo hilo kwa kutafuta wafadhili ameahidi mwaka huu ataanza ujenzi wa wodi za wagonjwa na hasa akina mama.
Akizungumzia jengo hilo jipya, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Dk Festo Bugange amesema kukamilika kwake kutapunguza msongamano wa akina mama waliokuwa wakisubiri kwa muda mrefu kufanyiwa upasuaji.
Dk Bugange amesema jengo hilo lina vyumba viwili vya upasuaji tofauti na kimoja kilichokuwepo awali. Amesema sasa watahudumia wagonjwa wengi zaidi na kwa muda mfupi.
Amesema Hospitali ya Mwananyamala inahudumia wagonjwa kati ya 1,800 na 2,000 kwa siku. Pia, inahudumia wajawazito kati ya 1,500 na 2,000 kwa mwezi.
"Asilimia 25 ya wajawazito wanaokuja Mwananyamala wanahitaji kufanyiwa upasuaji, kwa hiyo walikuwa wanasubiri kwa muda mrefu lakini sasa tuna vyumba vya upasuaji vitatu," amesema Dk Bugange.
No comments:
Post a Comment