Saturday, 27 January 2018

Taliban watumia 'ambulance' iliojaa vilipuzi kuwaua watu 95 Afghanistan

Mlipuaji wa kujitolea mhanga amewaua takriban watu 95 na kuwajeruhi wengine 158 katika mji mkuu wa wa Afghanistan Kabul, kulingana na maafisa.

Washambuliaji waliendesha ambyulensi iliokuwa imejaa vilipuzi kupitia kizuiazi cha polisi hadi katika barabara ambayo ilikuwa imetengewa wafanyikazi wa serikali.

Kisa hicho kilitokea katika jumba la wizara ya maswala ya ndani na afisi ya Muungano wa Ulaya na baraza kuu la amani.

Kundi la wapiganaji wa Taliban linasema kuwa walitekeleza shambulio hilo ambalo ni baya zaidi katika kipindi cha mwezi mmoja.

Walioshuhudia wanasema eneo hilo ambalo lina majumba ya balozi nyingi pamoja na makao makuu ya polisi mjini humo, lilikuwa na watu wengi wakati bomu hilo lilipolipuka siku ya Jumamosi .

Maafisa wanasema kuwa idadi ya waliofariki inaendelea kuongezeka huku majeruhi wakipelekwa hospitalini kwa matibabu.
Shirika la kimataifa la msalaba mwekundi limesema kuwa utumizi wa 'ambulence' unakera.Wiki moja iliopita ,wapiganaji wa Taliban waliwaua watu 22 katika hoteli moja ya kifarahari mjini Kabul.

Hili ndilo shambulizi baya zaidi kuwahi kufanyika mjini Kabul katika kipindi cha miezi kadhaa.

Mnamo mwezi Oktoba, watu 176 waliuawa katika shambulio la bomu mjini Afghanistan katika kipindi cha wiki moja.

Vikosi vya maafisa wa usalama vya Afghanistan vimeshambiliwa pakubwa na wapiganaji wa Taliban ambao wanataka kuweka sheria ya kiislamu katika taifa hilo.

Mnamo mwezi Mei, takriban watu 150 waliuawa na mpiganaji wa kujitolea mhanga mjini Kabul.

Kundi la wapiganaji wa Taliban walikana kutekeleza shambulio hilo lakini serikali ya Afghanistan inasema kuwa kundi la Haqqani ambalo ni mshirika wake lilitekeleza shambulio hilo kupitia usaidizi wa Pakistan.

Pakistan imekana kusaidia kundi lolote la wapiganaji linalotekeleza mashambulizi nchini Afghanistan .

Mwezi huu, Marekani ilikatiza usaidizi wake wa usalama kwa Pakistan, ikisema kuwa taifa hilo limeshindwa kuchukua hatua dhidi ya makunni ya kigaidi katika ardhi yake.


No comments:

Post a Comment