Timu ya Mbeya City
Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania kupitia Mkurugenzi wa Ligi Boniface Wambura imetangaza kuipiga faini ya jumla ya shilingi milioni moja klabu ya Mbeya City kwa makosa mawili tofauti.
Wambura amebainisha hayo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam na kusema timu hiyo ilitenda kosa la kutumia mlango usio rasmi kuingilia uwanjani katika mechi iliyofanyika Januari 1,2018 Jijini Mbeya ambapo kitendo hicho ni kosa kwa mujibu wa kanuni za ligi kuu na kutozwa laki 5 kama adhabu yao.
Aidha, Wambura alisema Kamati iliiagiza Sekretarieti ya Bodi ya Ligi kutoa waraka kwa wamiliki wa viwanja kuhakikisha timu zote zinaingia uwanjani kwa kutumia milango rasmi nasio vinginevyo.
Mbali na hilo, Wambura amesema Klabu hiyo pia imepigwa faini ya laki 5 kutokana na mashabiki wake kuingia uwanjani na kumzonga mwamuzi kwa madai alikataa kutoa 'penalti' kwa timu hiyo.
Kwa upande mwingine, Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania kupitia Mkurugenzi wa Ligi Boniface Wambura imetangaza kumfungia kocha wa timu hiyo Ramadhani Mwazurimo mechi mbili na kupigwa faini ya laki 5 kutokana na kutoa lugha ya kashfa katika mechi ya Tanzania Prisons dhidi ya Mbeya City iliyochezwa Januari 14, 2018 kwenye uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
No comments:
Post a Comment