NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’ amewasihi wananchi wa Tanzania kuendelea kuwaombea Dua na visomo mbali mbali Askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) wanaouawa wakilinda Amani katika nchini mbali mbali ikiwemo DRC Kongo.
Pia ameliomba Jeshi hilo pamoja na familia za ndugu wa marehemu Askari 10 waliofariki waliofariki siku za hivi karibuni wakilinda Amani Kongo, kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu.
Wito huo ameutoa leo mara baada ya kumalizika shughuli ya kisomo cha Khitma na Dua ya pamoja ya Arubaini ya kuwaombea marehemu hao iliyoandaliwa na Kamati ya Amani Kitaifa Zanzibar huko katika Msikiti wa Noor Muhammad (SAW) kwa Mchina Mwanzo Zanzibar.
Dk.Mabodi ameeleza kwamba Askari hao watakumbukwa daima kwa mchango wao wa kutetea na kulinda maisha ya Waafrika katika Nchi ya Kongo ambapo walikuwa wakiiwakikisha Tanzania kupitia Jeshi la Pamoja la Umoja wa Mataifa lililopo nchini humo kwa ajili ya kulinda Amani.
Aliwambia wananchi kuwa Mashujaa hao hakuna cha kuwalipa kwa sasa kwani wamepoteza uhai wao kutokana na uzalendo uliotukuka hivyo kilichobaki ni kuwaombea Dua wao Mwenyezi Mungu awapumzishe pahala pema peponi Amini na kuziombea familia zao ziendelee kuwa na subra.
Amefafanua kuwa msiba huo mzito ni sehemu ya Askari wa Majeshi mbali mbali ya Ulinzi na Usalama nchini wanaoendelea na kazi zao za kawaida wawe imara Kifkra na Kimwili bila kukata tamaa ili kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa Kituo kikuu cha Amani Barani Afrika na Duniani kwa ujumla.
Akizungumzia matunda ya kulinda misingi ya Amani nchini Dk.Mabodi amesema ni kuwepo kwa maendeleo katika Nyanja mbali mbali za Kiuchumi, Kisiasa na Kijamii.
“Wananchi tulinde tunu ya Amani na Utulivu tuliokuwa nao katika Taifa letu, ili tuweze kuwa Mabalozi wazuri wa kulinda Amani kwa nchi jirani na Mataifa mengine.”, amesisitiza.
“Nawapongeza Kamati ya Amani ya Taifa Zanzibar kwa maandalizi yao mazuri ya kuandaa shughuli ya kuwaombea Dua kubwa kama hii vijana wetu waliouwawa na watu wanaosadikiwa kuwa Waasi huko Nchini Kongo.”, amesema Dk.Mabodi.
Aidha ameeleza kuwa wananchi wanatakiwa kujenga utamaduni wa kuenzi Amani na Utulivu, uliopo nchini kwa lengo la kuepuka machafuko na migogoro isiyokuwa ya lazima nchini.
Naye Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Hussein Mwinyi, amewashukru wananchi mbali mbali waliojitokeza katika Khitma hiyo kwa lengo la kuwaombea Dua Marehemu Askari hao.
Amesema licha ya Tanzania kuwapoteza Mashujaa hao bado Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) litaendelea kuwa imara na kulinda mipaka na kushiriki harakati mbali mbali za kulinda amani hata nje ya Tanzani kwa lengo la kudumisha mahusiano mema na nchi nyingine Duniani
No comments:
Post a Comment