Friday, 24 November 2017

Viongozi Simba wataka Okwi aangaliwe zaidi


KUFUATIA kinara wa mabao Ligi Kuu Bara, Emmanuel Okwi kuwa majeruhi wa enka, uongozi wa klabu hiyo, umetoa rai kuhakikisha mchezaji huyo anapewa uangalizi wa hali ya juu kuona anafanikiwa kupona haraka kutokana na umuhimu wake katika kikosi hicho.

Okwi ndiye anayeongoza kwa kufunga mabao kwenye ligi kuu kwa sasa kutokana na kuwa na mabao nane akifuatiwa na Obrey Chirwa wa Yanga na Mohamed Rashid wa Tanzania Prisons ambao wote wana mabao sita.

Okwi alipata majeraha ya enka kabla ya mechi dhidi ya Prisons ya Mbeya ambapo kwa sasa anaendelea na matibabu.

 Taarifa kutoka Simba zinaeleza kwamba uongozi wa timu hiyo umemkabidhi jukumu Dk Yasin Gembe kuhakikisha anakuwa na uangalizi wa hali ya juu kwa mchezaji huyo kutokana na majeraha aliyonayo.

 “Uongozi umetaka Okwi awe chini ya uangalizi wa dokta kutokana na majeraha aliyonayo, kwa kuwa ndiye kinara wa mabao, hivyo ni vyema akaangaliwa ili aweze kupona kwa haraka na kurejea mzigoni,” alisema mtoa taarifa huyo.

 Simba inaongoza msimamo wa ligi kwa kuwa na pointi 22 huku Yanga ikiwa nafasi ya tatu kwa kuwa na pointi 20 ambapo timu zote zimeshuka dimbani mara 10, hali ambayo inaonyesha ni jinsi gani ligi imekuwa ngumu.

Sanchez, Buffon wanukia Kombe la Dunia



Bado kuna tumaini dogo kwa Italia au Chile kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia nchini Russia, yote ni kwa sababu ya muswada uliopelekwa katika Bunge la Peru utakaofanya Shirikisho la Soka la nchi hiyo kujiaonda moja kwa moja Fifa.

Chile ‘La Roja’ ilipoteza nafasi hiyo baada ya kufungwa 3-0 na Brazil katika siku ya mwisho na timu hiyo kumaliza nafasi ya sita, Wakati Italia wenyewe walifungwa bao 1-0 na Sweden katika mchezo wa mtoano na kuaga mashindano hayo.

Tofauti na Peru iliyofanikiwa kufuzu kwa fainali za mwakani baada ya kushinda 2-0 dhidi ya New Zealand.

Hata hivyo, Peru ‘Libero’ sasa wanaweza kupoteza nafasi hiyo, endapo serikali itaingilia masuala ya soka jambo litakalofanya Peru kupoteza tiketi yake ya kucheza Kombe la Dunia.

Mazingira hayo  yanafungua mlango kwa timu za Italia au Chile kupata nafasi ya kufuzu kwa fainali za mwakani

Kumbe mpango wa Kane ni kuvunja rekodi ya Shearer



Mshambuliaji nyota wa Tottenham Hotspurs, Harry Kane amesema anataka kufunga mabao katika kila mchezo.

Kane amefunga mabao 29 katika Ligi Kuu England na mkakati wake ni kufikia rekodi ya nguli wa zamani wa England Alan Shearer.

Nahodha huyo wa zamani wa England ana rekodi ya kufunga mabao 36 alipokuwa mchezaji wa Blackburn Rovers mwaka 1995.

Kane ametoa kauli hiyo wakati Spurs leo itakuwa ugenini kumenyana na West Brom katika mchezo wa Ligi Kuu England kwenye Uwanja wa Wembley.

 “Nilikosa baadhi ya mechi kutokana majeraha. Nilicheza michezo miwili au mitatu,” alisema nahodha huyo wa England.

Mshambuliaji huyo alidokeza anataka kufunga kila mchezo katika mechi tisa zilizobaki kabla ya mwezi ujao. Kane alifunga bao katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya walioshinda mabao 2-1 dhidi ya Borussia Dortmund, Jumanne iliyopita.

Mtoto wa Mfalme Saudia asema Hayatollah ni 'Hitler' mpya



Mwanamfalme wa Saudia amemtaja kiongozi wa kidini wa Iran kuwa 'Hitler' mpya wa eneo la mashariki ya kati huku kukiwa na wasiwasi kati ya mataifa hayo mawili.

Akitaja kuongezeka kwa ubabe wa Iran katika eneo hilo, Mohammed Bin Salman amesema kuwa ni vyema kuzuia yaliotokea barani Ulaya katika eneo la mashariki ya kati.

Saudia na Iran ni wapinzani na wamekuwa wakishutumiana kwa kuchochea ukosefu wa uthabiti katika eneo la mashariki ya kati.

Hatahivyo hakuna tamko lolote liliotolewa na Iran kufuatia matamshi hayo ya hivi karibuni.

Akizungumza na gazeti la The New York Times , Mohammed bin Salman alisema kuwa Iran haiwezi kuruhusiwa kusambaza ushawishi wake.

''Tulijifunza kutoka Ulaya kwamba kujionyesha kwamba wewe ni mtu mzuri hakufanikiwi''.
''Hatutaki Hitler mpya wa Iran kurudia yaliotokea barani Ulaya katika eneo la mashariki ya kati'', alisema akimtaja kiongozi wa kidini wa Iran Ayatollah Ali Khamenei.

Mohammed bin Salman, ambaye ndio mtawala mkuu wa ufalme huo amekuwa na msimamo mkali dhidi ya Iran tangu alipochukua mamlaka katika kipindi cha miaka miwili iliopita.

Mapema mwezi huu ,aliishutumu Iran kwa kile alichosema ni uchokozi wa kivita akiilaumu kwa shambuio la kombora lililolenga mji mkuu wa Saudia, Riyadh, na waasi katika taifa jirani la Yemen.
Iran imekana kwamba ilihusika.

Mastaa kibao kupamba kilele cha Fiesta kesho



MSIMU wa shamrashamra za muziki na kitamaduni katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati wa Tigo Fiesta 2017, ulio na kauli mbiu ya ‘Tumekusoma’, unatarajiwa kuhitimishwa kesho kwenye viwanja vya Leaders Club, Dar es Salaam, ukihusisha wasanii zaidi ya 18.

Akizungumza tamasha hilo Kaimu Mkurugenzi wa Masoko wa Tigo, William Mpinga, alisema kuwa, kwa mara ya kwanza katika historia ya miaka 16 ya tamasha hilo, Tigo Fiesta ilikuwa imewashirikisha wasanii wa Kitanzania pekee.

“Kilele cha msimu wa Fiesta 2017 kitawahusisha wasanii wa Kitanzania pekee. Tigo imejikita kuleta mageuzi makubwa kwa kuinua vipaji vya wasanii wa Kitanzania kama njia mojawapo ya kukuza sanaa na ajira kwa vijana nchini. Tumewakutanisha wasanii wetu maarufu na mashabiki wao katika mikoa yote 17 tuliotembelea na kuwajengea uwezo wa kutumbuiza laivu mbele ya halaiki kubwa ya watu,” alisema Mpinga.

Alisema kuwa, kupitia Fiesta 2017, wameibua vipaji vya muziki katika mikoa mbalimbali kupitia shindano la kuimba la Supa Nyota, ambapo washindi watapata fursa ya kutumbuiza katika kilele cha msimu kesho.

“Kununua tiketi ni rahisi. Fuata utaratibu wa kawaida wa kutuma pesa na tuma Sh 9,000 kwenda namba ya TigoPesa 0678 888 888. Hapo hapo utapokea ujumbe mfupi wa SMS unaothibitisha manunuzi yako ya tiketi. Hifadhi huo ujumbe mfupi. Baadaye utapokea maelekezo ya jinsi na wapi pa kwenda kuchukua tiketi yako. Bei halisi ya tiketi getini ni Sh 10,000,” alisema Mpinga.

Mratibu Mkuu wa Kamati ya Maandilizi ya Fiesta 2017, Sebastian Maganga, aliwataja wasanii watakaotoa burudani kesho katika tamasha hilo kuwa ni Ali Kiba, Aslay, Ben Pol, Barnaba, Chege, Darasa, Dogo Janja, Jux, Fid-Q, Rostam (Roma na Stamina), Rich Mavoko na Nandy.

Wengine ni Mr Blue, Vanessa Mdee, Maua Sama, Zaiid, Lulu Diva, Mimi Mars, Rosa Ree, Chin Beez, Nyandu Tozi, Nedy Music, Ommy Dimpoz, Bright, Weusi (Joh Makini, G-Nako na Nikki wa Pili) na wengineo.

Alisema kuwa, tamasha hilo kwa mwaka huu limezunguka katika mikoa ya Arusha, Kahama, Musoma, Mwanza, Tabora, Dodoma, Iringa, Songea, Njombe, Sumbawanga, Kigoma, Morogoro, Tanga, Mbeya, Moshi na Mtwara.

Wavuvi walia na usalama wao kazini





BAADA ya uwepo wa taarifa za wavuvi wilayani Rorya Mkoa wa Mara kuvamiwa na kunyang’anywa zana zao za kazi na samaki na maharamia wakiwa majini ndani ya Ziwa Victoria, wito umetolewa kwa Serikali kupitia Jeshi la Polisi kitengo cha majini kuimarisha ulinzi.

Wito huo ulitolewa na wananchi mbalimbali wanaojishughulisha na uvuvi katika Ziwa Victoria wilayani hapa wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, kukagua hali ilivyo.

Mmoja wa wananchi wanaojishughulisha na shughuli za uvuvi katika mwalo wa Nyang’ombe uliopo Kata ya Nyamagaro wilayani hapa, Richard Marwa, akizungumza kwa niaba ya wenzake alimwambia Naibu Waziri kwamba wanateseka sana wakati wakitekeleza shughuli zao kutokana na majambazi kutoka nchi jirani ya Uganda kuwapiga na kuwanyang’anya samaki.

“Tunaiomba Serikali kuingilia kati suala hili la wavuvi wa Tanzania kuvamiwa na majambazi kutoka nchi jirani ya Uganda huku wakitunyang’anya samaki na kutupiga na wengine hata kuuawa,” alisema Marwa.

Suala hilo liliongezewa uzito na Mbunge wa Jimbo la Rorya, Lameck Airo (CCM), ambaye alisema tatizo hilo ni la muda mrefu ambapo aliiomba Serikali kusikia kilio cha wananchi wake kwa kuongeza ulinzi ndani ya Ziwa Victoria ili kuondoa kero hiyo.

Naye Mkuu wa Kikosi cha Polisi Wanamaji Shirati Wilaya ya Rorya, Yusuph Juma, alisema kikosi chake kinazidiwa kwa  sababu hawana vifaa vya kutosheleza mahitaji na vilivyopo havifanyi kazi kutokana na kukaa muda mrefu bila kutumika.

Akijibu hoja hizo za wananchi, Naibu Waziri, Mhandisi Hamad Masauni, alisema Serikali ipo katika mashauri kuhakikisha ulinzi wa majini unaimarishwa kupitia Jeshi la Polisi huku akiahidi kukitafutia boti nyingine kikosi cha wanamaji Shirati ili kuongeza ufanisi katika shughuli zao.

“Tumekubaliana kuwaombea boti itakayokuwa na uwezo wa kwenda zaidi ya kilomita 20 kwa saa ili kuimarisha ulinzi majini hususani kwa wavuvi w

Lowasa asisitiza hana mpango wa kurudi CCM



WAZIRI Mkuu wa Zamani na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ameweka wazi tuhuma za madai ya kurejea Chama Cha Mapinudizi (CCM).

Juzi kupitia mitandao ya kijamii, kulikuwa na ujumbe wenye jina la Mrisho Gambo akidai amepokea ujumbe kutoka Monduli uliokuwa na ombi  kubwa moja.

Ujumbe huo uliokuwa umeandikwa kwenye ujumbe mfupi wa maneno, ulidai Mrisho ameombwa amuombee Mzee wa Monduli kwa Rais Magufuli ili akubali kumuona na yeye yupo tayari kurudi nyumbani kama rais atakubali kumuona.

Akizungumza na mamia ya wananchi wa Kata ya Makabi katika Halmashauri ya Wilaya ya Meru, wakati wa kampeni za kumnadi mgombea udiwani, Lowassa aliibuka na kudai hana mpango wowote wa kurejea CCM kama ilivyodai mitandao ya kijamii.

Aliendelea kudai kwenye mkutano huo uliohudhuriwa pia na Mbunge wa Jimbo  hilo, Nasari Sumari, kwamba taarifa hizo zinazodai kuwa kuna watu amewatuma kuomba arejee CCM, si za kweli zimelenga kupotosha umma.

Lowassa ambaye amekuwa akizungumza kwenye maeneo tofauti kunadi wagombea wa udiwani Kanda ya Kaskazini, alisisitiza kwamba taarifa hizi zimejaa uongo wa kutunga.

“Watu hawa wamekuwa wakitunga mambo mengi juu yangu, naomba niwaambie Watanzania sina mpango wala ndoto za kurudi CCM,” alisema Lowassa huku akishangiliwa na mamia ya wananchi waliojitokeza kwenye mkutano huo.

Lowassa aliyegombea kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na kufanikiwa kupata kura zaidi ya milioni sita, aliendelea kueleza kwamba watu hao wamekuwa pia wakisambaza uongo watu kuzuiliwa na Serikali kumtembelea nyumbani kwake.

“Yote haya ni maneno ya kutunga,” alisema Lowassa aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Monduli kabla ya kuhamia Chadema.

Kwa nyakati tofauti, Lowassa ameshiriki mikutano ya kampeni za kuwanadi wagombea udiwani katika Kata mbalimbali zilizopo mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.

Akiwa mkoani Arusha tayari amefanya mikutano katika Kata ya Moita Bwawani wilayani Monduli, Murrieti jijini Arusha, baadaye akaelekea mkoani Kilimanjaro akiwa huko msafara wake ulijikuta ukirushiwa mabomu ya machozi kwa lengo la kutawanya watu waliokuwa wamemzunguka.

Uchaguzi mdogo wa madiwani nchini unatarajiwa kufanyika Novemba 26, mwaka huu, baada ya madiwani waliokuwa wamepoteza sifa, huku wengine wakifariki na wengine kujiuzulu vyama vyao walivyokuwa wakivitumikia awali na hivyo kusababisha nafasi kuwa wazi.

BREAKING NEWS: Kafulila atua rasmi CCM


Baada ya kutangaza kujivua uanachama wa CHADEMA siku Jumatano, David Kafulila leo amekabidhiwa kadi ya CCM.

Kafulila amekabidhiwa kadi ya CCM na Katibu Mwenezi wa CCM, ndg Humphrey Polepole katika mkutano wa kumnadi mgombea wa udiwani wa chama hicho, Kata ya Mbweni jijini Dar es salaam.

Hapo awali Kafulila aliwahi kuwa mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendelo kisha kufuzwa baadae akajiunga na Chama cha NCCR Mageuzi ambapo alifanikiwa kuwa Mbunge wa Kigoma Kusini mwaka 2010-2015 na baadaye kurudi tena Chadema 2016 na hapo juzi jumatano alitangaza kukihama chama hicho kwa madai upinzani hauna nia ya kupambana na ufisadi.

Kwa upande wa mkewe ambaye ni Mbunge Viti Maalumu kupitia chama cha CHADEMA,Jesca Kishoa jana wakati akizungumza na wanahabari alipingana na kauli ya mumewe na kusema kwamba, mumewe anapaswa kusema ukweli na kwamba sababu alizozisema sizo zilizomuondoa ndani ya chama hicho huku akiongeza kwamba mume wake hana msimamo.

Kafulila amekabidhiwa kadi hiyo ya CCM iliwa imebaki siku moja kabla ya kuhitimishwa kwa kampeni za uchaguzi wa marudio ya nafasi za udiwani kwa Kata 43 ndani ya Tanzania

VIDEO: Majengo ya Lugumi yakosa Wateja, Docta Shika atajwa



Dar es Salaam. Jumba la kifahari la mfanyabiashara, Said Lugumi limekosa mteja wa kulinunua.

Katika mnada uliomalizika Leo mchana Novemba 24 Mbweni JKT, ulioendeshwa na Kampuni ya Udalali ya Yono, wanunuzi waliojitokeza wameshindwa kufikia bei elekezi
TAZAMA FULL VIDEO HAPA CHINI.... USIKOSE KUSUBSCRIBE

Mkurugenzi wa Kampuni ya Yono, Scholastika Kevela amesema wateja waliojitokeza wamefikia Sh510 milioni ambayo iko chini ya mategemeo.

"Tunahamia nyumba ya Upanga, kama atapatikana mteja leo tunaweza kurudi na tukamuuzia na masharti ni yaleyale kwamba lazima mteja akifika bei alipe hapa hapa asilimia 25 na asilimia 75 ndani ya siku 14," amesema Kevela

Nyumba hii imeshindwa kununuliwa kwa mara ya tatu baada Septemba 7 kujitokeza kama leo na Novemba 9 ambao unadaiwa ulivurugwa na 'Bilionea' Dk Louis Shika.

Tofauti na ulivyokuwa Novemba 9, leo kila aliyefika katika mnada huo alitakiwa kujiandikisha ikiwamo waandishi wa habari huku ulinzi ukiwa umeimarishwa  zaidi .

Zimbabwe: Shamba la Grace Mugabe lavamiwa na wanakijiji




Mamia ya wanakijiji katika shamba la Arnold katika kijiji cha Mazowe nchini Zimbabwe walivamia shamba la Grace Mugabe ili kusheherekea kung'atuliwa mamlakani kwa kiongozi huyo waliyedai amekuwa akiwanyanyasa na kuwafanya kuwa masikini kwa lengo la kuimarisha mali ya familia yao.

Aliyekuwa rais wa Zimbabwe Robert Mugabe alijiuzulu siku ya Jumanne hatua iliozua sherehe kubwa miongoni mwa raia wa taifa hilo.

Wanakijiji cha Mazowe ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakizozana na familia hiyo ya Mugabe kuhusu shamba hilo la Arnold wamesema kuwa wanataka kuonyesha ahsante yao kwa wale wote waliofanikiwa kumng'oa madarakani Mugabe.

Kwa saa kadhaa wanakijiji hao waliobeba mabango waliimba na kucheza densi kwa nyimbo za uhuru huku wengine wakikashifu tamaa ya bwana Mugabe na kuandamana nje ya lango la nyumba ya mayatima la Mazowe wakitaka haki kabla ya kuandamana katika kituo cha maduka pamoja na wenzao wanaosherehekea kuanguka kwa Mugabe.

Wengine hususan wazee walikionyesha chombo cha habari cha Newsday majeraha waliopata baada ya kupigwa na maafisa wa polisi.

Waliionya familia ya Mugabe kutoingia katika shamba lao.

''Kwa sababu ya Grace na Mumewe tulilazimika kuishi katika shamba la Arnold kama wafungwa.Walibomoa nyumba zetu kila mara tulipojaribu kujenga.Walifurahia tulipolala nje na wajukuu zetu'', alisema Stella Nikisi mwenye umri wa miaka 65 akionyesha jeraha alilopata katika mguu baada ya kushambuliwa na maafisa wa polisi.

Serikali ya Rwanda yatangaza kuwa ipo tayari kupokea wahamiaji 30 000 waliokumbwa na madhila nchini Libya


Kufuatia matendo ya unyanyasaji na ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Libya ambapo  wahamiaji haramu waliokuwa wakitaraji kusafiri kupitia Libya kuelekea barani Ulaya kujipata katika mnada, Rwanda  imetangaza kuwa ipo tayari kuwapokea wahamiaji 30 000 katika ardhi yake.

Moussa Faki Mahamat, kamishna mkuu wa Umoja wa Afrika katika ukurasa wake  wa Twitter amefahamisha kuwa amefurahishwa na  serikali ya Rwanda  kujitolea kuwapokea wahamiaji kutoka Libya na kuahidi kuwa ipo tayari pia kuandaa  safari za wahamiaji hao katika mataifa yao iwapo watakuwa tayari kurejea kwa hiari.


Marekani yatoa tahadhari kwa raia wake kusafiri kuelekea nchini Saudi Arabia



Marekani imewatahadharisha raia wake kusafiri kuelekea nchini Saudi Arabia na kusema kuwa lna vitisho kutoka katika makundi ya kigaidi kushambulia kwa makombora kutoka nchini Yemen.

Saudi Arabia kwa upande wake haikutoa taarifa yeyote kuhusu tahadhari hiyo iliotolewa na Marekani.

Tangazo lililotolewa limefahamisha kuwa vitisho vya mashambulizi dhidi ya mji wa Riyadh, Jeddah na Dhahran vinaendelea .

Makundi ya kigaidi ikiwemo kundi la wanamgambo wa Daesh nchini Iraq na Syria yalilenga ofisi za serikali ya Saudi Arabia, miskiti na meneo mengine mengi ambayo raia wa kigeni wakiwemo wamarekani huwa wanapenda kutembelea.

Jeshi la Polisi la Saudi Arabia lilifaulu kuzuia mashambulizi ya kigaidi  yaliokuwa yakilenga mskiti wa  Macca na kupelekea kukatwa kwa baadhi ya viongozi wa Daesh.

Dk Shika apokewa ‘kifalme’ Shinyanga



Kahama. Dk Louis Shika ‘bilionea’ aliyejizolea umaarufu baada ya kuibuka katika mnada wa kununua nyumba za mfanyabiashara Said Lugumi ametua mjini Kahama na kupokewa na watu wengi.

Mapokezi ya Dk Shika aliyetua mjini hapa kuwa mgeni rasmi katika mahafali ya Chuo cha Afya cha Kahama (Kahama College of Health Science), yameongozwa na msururu wa magari zaidi ya 50 na kupita kwenye mitaa mbalimbali kabla ya kuelekea chuoni, Kata ya Mwendakulima, nje kidogo ya mji wa Kahama.

Mapokezi hayo leo Alhamisi Novemba 23,2017 yameongozwa na Mkurugenzi wa chuo hicho, Yona Bakungile kuanzia uwanja wa ndege wa Buzwagi.

Ili kupata fursa ya kusalimiana na kuwapungia mikono mamia ya watu waliojipanga barabarani kumshuhudia baada ya kupata habari zake, Dk Shika alipanda gari la wazi, jambo lililofanya hata baadhi ya watu wenye shughuli zao maeneo alikopita kuzitelekeza kwa muda kwenda kumshuhudia.

Mwenyeji wake alonga
Akizungumza na Mwananchi sababu za kuamua kumwalika Dk Shika katika mahafali ya chuo chake, Bakungile amesema ni kutokana na utaalamu wake wa masuala ya tiba ya binadamu na umaarufu wake unaoendelea kuvuma nchini.

“Chuo changu kinatoa mafunzo ya afya ya binadamu; licha ya umaarufu wake nchini kwa sasa, Dk Shika ni miongoni mwa wataalamu katika fani ya utabibu ndiyo maana nimemwalika. Naamini atawashauri na kuwapa hamasa wahitimu na wanafunzi wanaoendelea,” amesema Bakungile

Dk Shika atangaza neema ya ada
Akihutubia mbele ya umati uliojitokeza, wakiwemo wananchi waliofuata msafara wake kutoka mjini umbali wa zaidi ya kilomita tatu kutoka chuoni, Dk Shika ameahidi kulipa ada na gharama za masomo kwa wanafunzi ambao wana uwezo kimasomo lakini wazazi au walezi wao hawawezi kuwalipia.

“Natambua umuhimu wa masomo ya afya na ughali wa malipo yake kwa Watanzania wenye kipato cha chini; nitawalipia wanafunzi wote wenye uwezo darasani lakini wazazi au walezi wao hawawezi kugharamia masomo yao,” ameahidi Dk Shika.

Amesema uamuzi wake unalenga kuhakikisha Taifa linakuwa na wataalamu waliobobea katika taaluma ya utabibu.

Mkurugenzi wa kituo cha huduma ya mawasiliano ya mtandao cha Mary Internet, Mary Patrick ambaye ni kati ya walioshangazwa na ujio na msafara wa magari ametaka Dk Shika kutumia vyema umaarufu wake kusaidia jamii.

Mwananchi: