Thursday, 8 February 2018

Wabunge ANC wakutana kumjadili Zuma

Afrika Kusini.  Kamati ya Bunge ya Chama cha ANC (caucus) inakutana mchana huu katika kikao cha siri ambacho hata hivyo ajenda zake hazikuwekwa wazi kwa waandishi wa habari.

Kamati hiyo inakutana huku kukiwa na shinikizo linalomtaka Rais Jacob Zuma kuachia madaraka.

Duru za habari zinasema kiongozi mkuu wa ANC, Cyril Ramaphosa ndiye atayehutubia kikao cha kamati hiyo inayokutana mjini Cape Town.

Maofisa wa chama hicho hawakuwa tayari kueleza ajenda muhimu za mkutano huo wa dharura mbali ya kusisitiza kuwa ni mkutano wa ndani.

Hata hivyo, taarifa zinasema wabunge hao huenda wakajadili suala la kuondoka madarakani kwa Rais Zuma na kipindi cha mpito kuelekea katika uchaguzi mkuu mwakani.

Awali, Ramaphosa amesema amekuwa akifanya  mazungumzo ya moja kwa moja na Rais Zuma kuhusiana na kipindi cha mabadiliko na masuala yanayohusu wadhifa wa rais wa nchi hiyo.

Zuma ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2009 na ambaye anakabiliwa na madai ya ufisadi amekuwa na nafasi finyu ya ushawishi tangu Ramaphosa arithi nafasi ya kiongozi mkuu wa ANC.

Katika taarifa, Ramaphosa amesema yeye na Zuma wanatarajia kukamilisha mazungumzo na waifahamishe nchi kuhusiana na mazungumzo katika siku zijazo.

 Amesema mazungumzo hayo ni nafasi ya kutafuta suluhisho bila kuleta mgawanyiko nchini humo.

No comments:

Post a Comment