Kampuni ya Simu za Mkononi ya Tigo imepunguza gharama za kupiga simu na kutuma ujumbe mfupi wa maandishi kitaifa na kimataifa kwa asilimia 27.5.
Takwimu zilizotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha kuwapo kwa punguzo hilo katika robo ya nne ya mwaka iliyoishia Desemba 2017 ikilinganishwa na robo ya tatu ya mwaka ulioishia Septemba.
Ripoti ya robo ya tatu ilionyesha kuwa Tigo ndiyo mtandao wenye gharama kubwa Tanzania katika kupiga simu na kutuma ujumbe mfupi kitaifa na kimataifa jambo ambalo limekuwa tofauti na robo ya nne ya mwaka.
Katika robo ya tatu ya mwaka wateja wa Tigo walikuwa wakilipia Sh360 kwa dakika (kabla ya VAT) katika kupiga simu ndani ya mtandao ambayo imeshuka hadi kufikia Sh261 katika robo ya nne ya mwaka, ikiwa ni pungufu ya Sh99 sawa na asilimia 27.5.
Hata hivyo, kushuka kwa gharama za kupiga simu ndani ya mtandao katika robo ya nne, takwimu zinaonyesha kuwa tozo za Tigo bado zipo juu ya wastani wa gharama za kupiga simu ambazo ni Sh249 kwa dakika.
Katika kupiga simu nje ya mtandao wateja wa Tigo walikuwa wakilipia Sh480 kwa dakika katika robo ya tatu ya mwaka ambayo imeshuka hadi kufikia Sh348 ambayo ni sawa na pungufu ya asilimia 27.5.
Licha ya kuwapo kwa punguzo hilo, tozo hiyo bado ipo juu ya wastani wa gharama za kupiga simu nje ya mtandao ambazo ni Sh329 kwa dakika.
Katika kupiga simu Afrika mashariki wateja wa Tigo walikuwa wakilipia Sh1,022 kwa dakika katika robo ya tatu ya mwaka ambayo imepungua hadi kufikia Sh739 katika robo ya nne ya mwaka ikiwa ni pungufu ya Sh283 sawa na asilimia 27.7.
"Kupungua kwa gharama hizo kumeifanya Kampuni ya Tigo kuwa miongoni mwa kampuni zinazotoza tozo iliyo chini ya kiwango cha wastani ya kupiga simu Afrika ya Mashariki ambayo ni Sh745 kwa dakika,"amesema.
Katika kupiga simu kimataifa, Tigo ilikuwa ikitoza Sh1,737 katika kupiga simu kwa dakika katika robo ya tatu ya mwaka ambayo imepungua hadi kufikia Sh1,258, ikiwa ni pungufu ya Sh479 sawa na asilimia 27.6.
Kupungua kwa gharama hizo kunaifanya Tigo kuwa chini ya wastani wa tozo za kupiga simu kimataifa ambayo ni Sh1,273.
Kutuma ujumbe mfupi
Katika kutuma ujumbe ndani ya mtandao, Kampuni ya Tigo imepunguza gharama hadi kufikia Sh51 katika robo ya nne ya mwaka kutoka Sh70 iliyokuwapo katika robo ya tatu ya mwaka, hiyo ni sawa na pungufu ya Sh19 sawa na asilimia 27.14.
Tozo hizo za kutuma ujumbe mfupi ziko sawa na wastani uliowekwa wa Sh51 kwa kila ujumbe.
Katika kutuma ujumbe mfupi wa maandishi kimataifa gharama imepungua hadi kufikia Sh156 katika robo ya nne ya mwaka kutoka Sh 215 ya robo ya tatu ya mwaka ikiwa ni pungufu ya Sh59 sawa na asilimia 27.4.
Gharama hizo ziko juu ya wastani wa tozo za kutuma ujumbe nje ya nchi ambayo ni Sh95.
No comments:
Post a Comment