Wednesday, 7 February 2018

Msigwa amfungukia Kigwangalla Bungeni

Mbunge wa Iringa Mjini kwa tiketi ya CHADEMA, Mhe. Peter Msigwa amefunguka na kumchana Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangala na kudai kuwa anafanya kazi kwa mizuka na mihemko na kuisumbua sekta ya Utalii na Maliasili nchini.

Msigwa amesema hayo wakatii alipokuwa akichangia bungeni taarifa ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji, mjini Dodoma na kudai kuwa Mawaziri vijana wamekuwa na mihemko.

"Niwashauri hawa Mawaziri vijana fursa 'opportunity is atrracted by talent, skills, perfomance and abillity. Show your talent and abillity people will love you' hawa Mawaziri wa zamani hawa kwa mfano Lukuvi, Tizeba tunawaona wakijibu hoja wanajibu hoja siyo za kimihemko kiasi kwamba unaridhika hata Waziri akikujibu unapenda lakini Mawaziri vijana wengi mnaonekana mnayofanya katika Serikali hii kiasi kwamba Serikali ijayo muonekane hamna tija" kwa sababu mna mihemko sana"

Mbali na hilo Msigwa alikwenda mbali zaidi na kumnyooshea mkono Waziri wa Maliasili na Utalii na kudai amekuwa na maamuzi ya ajabu jambo ambalo linapelekea kiongozi huyo kuivuruga Wizara hiyo.

"Utalii huu umejengwa kwa muda mrefu sana na akitokea mtu mmoja anaamua kufanya tu kwa kutafuta umaarufu atauvuruga kwa muda mfupi sana, Utalii kwenye pata la taifa unaingiza asilimia 20 na forex ni kubwa inatokana na utalii kwa hiyo hicho si kitu kimoja mtu anaweza kuamka leo anasema nimeharibu na hii diplomasia ya kiuchumi inategemea sana na kutabirika, wawezekaji huko nje wanataka kuona kunatabirika wao kufanya biashara zao. Haiwezekani huyu Waziri anatoa amri mpaka mapolisi wanamkataa anashindwa hata kuwasiliana na Waziri wake wa Mambo ya Ndani, huyu huyu Waziri anatoa amri anapingana na Waziri wa Ardhi, huyu huyu Waziri mmoja anapingana na Waziri wa Uvuvi hatuwezi kuwa na Mawaziri ambao wanakuwa na mizuka na kufanya kazi kwa mizuka wote kama tunalipenda taifa letu tufanye kazi kwa kupendana" alisisitiza Mchungaji Msigwa

No comments:

Post a Comment