Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt Rehema Nchimbi amewataka viongozi wa vijiji na kata mkoani humo kuhakikisha wanatunga sheria ndogo ya kunyonyesha ndani ya miezi minne ili kuondokana na tatizo la ukosefu wa lishe kwa watoto.
Dkt Nchimbi ametoa agizo hilo Juzi Ijumaa kwenye hafla ya kukabidhiwa vifaa vya kutambua hali ya lishe kwa watoto na akinamama wajawazito katika kijiji cha Saranda wilayani Manyoni.
“Kunyonyesha ni lazima, Wenyeviti wa vijiji na kata hakikisheni mmetunga sheria ndogo kwa ajili ya kudhibiti akinamama wote wasionyonyesha watoto wao kulingana na taratibu za afya,”amesema Dkt. Nchimbi.
Mhe Nchimbi amelazimika kutoa agizo hilo baada ya kusomewa taarifa inayoonesha kuwa ni asilimia 54 pekee ya watoto mkoani Singida ndio hubahatika kunyonyeshwa maziwa ya mama pekee kwa kipindi cha miezi sita.
Akisisitizia suala hilo Dkt. Nchimbi amesema kuwa ulazima huo usibakie kuwa ni wa majukwaani tu bali utekelezwe kisheria na atakayepatikana aadhibiwe, hata hivyo, mhakikishe adhabu hiyo haisababishi mama kumkimbia mtoto.
No comments:
Post a Comment