Wednesday, 7 February 2018

Hizi ndizo Njia tatu za kupunguza foleni Dar

Wakati Serikali ikiendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali kukabiliana na changamoto ya foleni jijini Dar es Salaam, Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (Jica) limekuja na mwarobaini wa tatizo hilo.

Timu ya wataalamu wa shirika hilo imefanya utafiti ulioonyesha njia mbalimbali zinazoweza kutumiwa kukabiliana na foleni kubwa, ikiwamo ujenzi wa reli.

Akizungumza wakati wa uwasilishaji wa mpangilio wa sekta ya usafirishaji katika Jiji la Dar es Salaam kwa mwaka 2018 hadi 2040, mwakilishi wa Jica nchini, Toshio Nagasa alisema kufikia mwaka 2040 wakazi wa jiji hilo watakuwa wameongezeka kutoka milioni sita hadi 12. Kutokana na ongezeko hilo Nagasa alisema ni muhimu kwa Serikali kuweka mazingira wezeshi ya usafiri ili kuwezesha sehemu zote za jiji kufikika kwa urahisi huku shughuli za uchumi zikiendelea.

“Kukabiliana na msongamano utakaojitokeza katika kipindi hicho ni muhimu Serikali ikafikiria kujenga miradi ya reli, ambayo inaweza kusafirisha watu wengi kwa pamoja, hii itasaidia kupunguza magari binafsi kuingia barabarani,” alisema.

Licha ya reli, mpango huo umeshauri kuwapo kwa barabara za juu katika makutano ya Morocco, Chang’ombe na Mwenge.

Kingine kilichoelekezwa katika mpango huo, ni uwapo wa miji midogo maeneo ya pembezoni ili kupunguza msongamano katikati ya jiji.

Kauli ya Serikali

Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Spora Liana alisema wataalamu hao wameshauri miji hiyo midogo iwekewe huduma zote za msingi ili watu wengi wasiende mjini. Alisema utekelezaji wa mradi huo utagharimu Sh19.1 bilioni ukihusisha ujenzi wa miundombinu.

Wakati huohuo, mkurugenzi wa Tanroads Mkoa wa Dar es Salaam mhandisi Patrick Mfugale alimweleza waziri wa Ujenzi na Usafirishaji wa Lesotho, Lehlohonolo Moramotse, kuwa mradi wa ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya barabara ya Mandela na Nyerere (Tazara) wenye thamani ya Sh95 bilioni, unatarajia kukamilika Mei na kutumika rasmi mwishoni mwa Oktoba. Waziri huyo yupo nchini na wataalamu wa wizara yake kujifunza namna ambavyo wenzao wanasimamia ujenzi, ukarabati na utunzaji wa barabara.

No comments:

Post a Comment