Waziri wa mambo ya ndani nchini, Mwigulu Nchemba leo ameongoza oparesheni ya kuteketeza jumla ya ekari sita za bangi zilizokuwa zimelimwa katikati ya msitu ndani ya kijiji cha Engalaoni wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Mwigulu akishirikiana na kamanda wa jeshi la polisi mkoani Arusha,(RPC)Charles Mkumbo pamoja na vikosi vya askari wa jeshi la polisi mkoani hapa walilazimika kuacha magari yao njiani na kutembea umbali wa kilomita 5 milimani kufika katikati ya msitu huo ambapo wamiliki wa mashamba hayo walitokomea kusikojulikana.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa zoezi hilo Mwigulu alisema kwamba serikali itaendelea na oparesheni pande zote za nchi na haitasita kuwakamata wahusika wote na kutaifisha magari yatakayotumika kusafirisha bangi.
Akizungumza na askari waliokuwa wakishiriki katika zoezi hilo Mwigulu mbali na kuwapongeza kwa kazi wanayofanya lakini aliwambia kwamba pamoja na kufanikiwa kuteketeza madawa ya kulevya yanayolimwa mashambani lakini waongeze juhudi pia katika kupambana na madawa ya kulevya yanayotengenezwa viwandani.
“Niwapongeze sana songeni mbele na kazi ya kukamata madawa yote ya kulevya mmefanya kazi kubwa sana ya kukabiliana na madawa ya kulevya yanayolimwa mashambani ongezeni bidii kukamata na yale yanayozalishwa viwandani,” alisema Waziri Mwigulu.
Hata hivyo, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Arusha(RPC),Charles Mkumbo alisema kwamba jumla ya ekari sita za mashamba ya bangi zimeteketezwa na kusisitiza kwamba oparesheni hiyo ni endelevu katika mkoa wa Arusha na wilaya zake.
Aidha Kamanda Mkumbo alifichua mbinu mpya wanayotumia wamiliki wa mashamba hayo kwamba kwa sasa wameamua kulima mashamba hayo katikati ya misitu kwa lengo la kujificha ili kukwepa mkono wa sheria.
“Walidhani kulima bangi katikati ya misitu hatutawakamat sisi tuna mbinu nyingi na hatutakubali kuona vijana wetu wanaharibikiwa kwasababu ya bangi.”
No comments:
Post a Comment