Wednesday, 7 February 2018

. Nassari: katika Jimbo langu kumeanza kuibuka migogogro juu ya michango

Arusha. Mbunge wa jimbo la Arumeru Mashariki (Chadema) Joshua Nassari, ameitaka Serikali kutoa tamko moja juu ya michango ya chakula shuleni kama ni halali ama la ili kuzuia migogoro ambayo imeanza kuibuka.

Akizungumza na Mwananchi leo Februari 7 Nassari amesema  katika jimbo lake kumeanza kuibuka migogoro juu ya michango ya chakula kwani kuna wazazi ambao walikuwa wamechangia mara baada ya shule kufunguliwa na sasa wanataka warejeshewe michango yao.

‘’Hili  suala limeleta utata mkubwa na mgongano baina ya walimu, Kamati za shule na wazazi, kwani  baadhi ya wazazi wameaminishwa kuwa Serikali imetoa fedha kugharamia mahitaji yote ya shule," amesema

Amesema  ni muhimu kuwepo na tamko moja ni michango gani, ambayo ni marufuku na ipi ambayo inakubalika na hivyo kuwekwa utaratibu mzuri wa kuikusanya.

Alisema anachofahamu ni kuwa Serikali, haijapiga marufuku michango ya chakula, bali kinachotakiwa ni wazazi kutoa kwa hiari yao baada ya kukubaliana katika vikao lakini jambo hili linapaswa kuelimishwa.

Waraka namba 3 wa mwaka 2016 juu ya suala la elimu bure, pia umeeleza jukumu la chakula cha wanafunzi kwa shule za kutwa na sare za shule ni la wazazi.

Diwani wa kata ya Imbaseni, Gabriel Mwanda alisema katika kata yake, kuna wazazi walichanga chakula shuleni, lakini kutokana na tamko la serikali la kuzuia michango wameanza kuidai.

"Hili ni tatizo, tumejaribu kuwaeleza wazazi juu ya umuhimu wa michango baadhi wameelewa na wengine bado hawajaelewa" amesema

Mwanda amesema ni ukweli ni kuwa fedha ambazo zinapelekwa shuleni, hazitoshi mahitaji yote lakini sintofahamu iliyopo sasa isipopatiwa ufumbuzi itaathiri sekta ya elimu.

"Suala la chakula kwa watoto  shuleni ni muhimu sana hivyo tumekuwa tukishauri wazazi kuchanga kwa hiari lakini watoto wasirejeshwe nyumbani kwa wazazi wao kwa kushindwa kuchangia chakula," amesema.

Katika shule nyingi wilaya ya Arumeru, kamati za shule zilikuwa zimepitisha mchango wa debe mbili za mahindi na kilo tano za maharage kwa ajili ya chakula na tayari shule zilipofunguliwa wazazi walichanga.

Hata hivyo, kutokana na kuibuka utitiri wa michango shuleni, hivi karibuni Rais John Magufuli alitangaza kupigwa marufuku walimu kupokea michango mashuleni na akawataka wazazi ambao wanataka kujitolea kupeleka michango yao kwa  wakurugenzi.

No comments:

Post a Comment