Askofu mstaafu wa Kanisa Anglikana, Donald Mtetemela amesema baadhi ya viongozi wa kanisa wanaweza kuwa chanzo cha migogoro kutokana na tamaa ya mali na madaraka.
Askofu Mtetemela amesema hayo leo Jumapili Februari 4,2018 wakati ya misa ya kuwekwa wakfu na kusimikwa Askofu mteule Jackson Sosthnes wa kanisa hilo Dayosisi ya Dar es Salaam.
Amesema migogoro makanisa ni kazi ya shetani anayevuruga huduma ya Mungu ili isifanikiwe, hivyo kuwa katika hali ya hatari muda wote.
Askofu Mtetemela amesema migogoro haiwahusu waumini wa kanisa hilo pekee bali makanisa yote.
“Migogoro ni njia ya shetani ili kudhoofisha huduma ya kanisa, kazi yake ni kuingiza watu wasiofaa ili waweze kuwa viongozi. Utakuta mtu amevaa ngozi ya kondoo kumbe mbwa mwitu na wengine wanaingiza maandiko ambayo si maneno yaliyoandikwa kwenye vitabu vya dini,” amesema.
Amesema migogoro huleta chuki na roho ya kulipiza kisasi.
Amemweleza Askofu Jackson kuwa kazi yake si nyepesi, hivyo anatakiwa awe imara.
Askofu Jackson anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Dk Valentino Mokiwa aliyeondolewa madarakani na uongozi wa juu wa kanisa hilo takriban mwaka mmoja uliopita.
No comments:
Post a Comment