Sunday, 4 February 2018

Hospitali ya Aga Khan yaandaa Kampeni kuhamasisha Wananchi kupima saratani ya Utumbo



Hospitali ya Aga Khan kwa kushirikia na Mpango wa Taifa wa Damu Salama imeandaa kampeni kuhamasisha wananchi kupima saratani ya utumbo ili kujihami na ugonjwa huo.

Upimaji wa saratani ya utumbo ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya saratani duniani ambayo huadhimishwa kila Februari 4.

Akizungumza leo Jumapili Februari 4,2018 daktari bingwa wa magonjwa ya saratani wa Hospitali ya Aga Khan, Dk Harrison Chuwa amesema hospitali hiyo imeamua kuhamasisha upimaji wa ugonjwa huo baada ya kuona kuna ongezeko la wagonjwa.

Amesema ili kujua kama una ugonjwa huo, kuna kipimo ambacho kinauzwa kwenye maduka ya dawa.

"Kipimo hiki unaweza kujipima mwenyewe ukiwa nyumbani, ukibainika kuwa na saratani ya utumbo ndipo unaweza kuwaona madaktari kwa uchunguzi zaidi," amesema.

Daktari bingwa wa magonjwa ya saratani wa hospitali hiyo, Dk Aleesha Adatia amesema ugonjwa huo unatibika iwapo mgonjwa atawahi kutibiwa.

"Wagonjwa wengi huwa wanafika hospitali wakiwa wamechelewa, tunashauri watu kujipima kwa kutumia kipimo hicho angalau mara moja kila mwaka," amesema.

Kuhusu dalili, Dk Adatia amesema ni kutoka damu wakati wa kujisaidia haja kubwa, kuchoka na kupungua uzito.

Ofisa kutoka Mpango wa Damu Salama Kanda ya Mashariki, Fatma Mjungu amesema wanashirikiana na hospitali hiyo kwa kuwa kuna mahitaji makubwa ya damu kwa wagonjwa wa saratani.

"Ndiyo maana tupo hapa wakati wenzetu wanahamasisha upimaji wa saratani ya tumbo sisi tunahamasisha watu wajitolee kuchangia damu," amesema.

Amesema asilimia 25 ya damu inayokusanywa na mpango huo inatumiwa na wagonjwa wa saratani.

Amesema asilimia 42 ya damu inayokusanywa na mpango huo inatumiwa na watoto, huku asilimia 21 ikitumiwa na akina mama.

"Hivyo, ongezeko la saratani ya utumbo inasababisha matumizi makubwa ya damu, tunaomba jamii ichangie damu," amesema.

No comments:

Post a Comment