Sunday 21 January 2018

Kocha wa Simba afunguka kuhusu Nicholas Gyan

Kocha msaidizi wa vinara wa ligi kuu soka Tanzania Bara Simba SC Masoud Djuma, ameweka wazi kuwa pamoja na kumpatia nafasi ya kucheza hivi sasa nyota wa timu hiyo kutoka Ghana Nicholas Gyan, lakini aliwahi kumwambia hajui kucheza.

Masoud  amesema baada ya kujiunga na Simba alimkuta Gyan na baada ya kumtazama kwenye mazoezi alimtamkia kuwa hawezi kucheza soka wala hafananii kuwa mchezaji lakini kwasasa Gyan amemjibu kwa vitendo.

"Nilimwita Gyan na kuzungumza naye na nikamwambia wewe si mchezaji, inakuwaje haupigi pasi, wala hautulizi mpira vizuri, kwa sababu haiwezekani mchezaji awe anakosa vitu hivyo, lakini kumbe mwenyewe kichwani alikuwa anafikiria kuwa  anarogwa," ameeleza Masoud.

Kocha huyo raia wa Burundi ameongeza kuwa baada ya kugundua kuwa Gyan anawaza hivyo alikaa naye na kumshauri kisha akampa nafasi ya kucheza na mwisho wa siku ameonesha kiwango kikubwa na amekuwa msaada kwa timu.

Masoud amekuwa akimtumia Gyan upande wa kulia kutokana na kasi yake ili kusaidia mfumo wake wa 4-4-2 ambao huwa unabadilika na kuwa 3-5-2 timu ikiwa inacheza hivyo Gyan mara nyingi husaidia kurudi kama mlinzi wa kulia na baadae kupanda kama winga.

No comments:

Post a Comment