NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndungulile, amesema wizara yake imeanza kukabiliana na changamoto ya watumishi wa Afya kwa kuomba kibali cha kuajiri.
Dk. Ndungulile alitoa kauli hiyo jana alipokuwa ziarani mkoani Mbeya baada ya kupokea taarifa ya wafanyakazi wa idara hiyo kutoka kwa Muuguzi Mkuu wa Mkoa, Elesia George, unakabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi wa idara hiyo.
Elesia alisema upungufu huo wa watumishi umepelekea vituo vya Afya na Zahanati za Serikali 59 mkoani humo kuongozwa na wauguzi kutokana na kutokuwa na madaktari.
Alisema hali hiyo inahatarisha afya za wananchi kutokana na uwezo mdogo wa wauguzi hao usioendana na majukumu wanayopewa.
Alisema uhaba wa watumishi hao unapelekea wauguzi wanaopewa majukumu hayo kufanya kazi nyingi kwa wakati mmoja na hivyo kuwapunguzia ufanisi wa kazi.
Aliomba Serikali iajiri watumishi wa kada hiyo ili kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi na kuwapunguzia mzigo wauguzi ambao wanapewa majukumu wasiyokuwa na uwezo wa kuyamudu.
“Ili huduma za afya ziwe bora ni vizuri tukawa na professionals (wanataaluma), kwenye mkoa wetu tuna upungufu mkubwa wa matabibu hivyo unakuta wauguzi wanafanya kazi zote, tunaomba kwenye kama kuna ajira mpya tunaomba kada hii izingatiwe,” alisema Elesia.
Baada ya maelezo hayo ya Muuguzi Mkuu wa Mkoa, Naibu Waziri Dk. Ndugulile alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo, lakini akasema wizara yake tayari imeshaanza kuchukua hatua kwa kuomba kibali cha kuajiri watumishi wapya.
Alisema wanakusudia kuajiri watumishi hasa kwenye maeneo nyeti ili kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya Afya nchini na hata kuwapunguzia kazi baadhi ya watumishi ambao wana majukumu mengi wakati mwingine.
“Wekeni masanduku ya maoni kwenye maeneo yote ambayo yana mkusanyiko mkubwa wa watu, ili mjuwe malalamiko ya wananchi na myashughulikie na yale mnayoshindwa mnayaleta wizarani tunayashughulikia,” alisema Dk. Ndugulile.
Pia Dk. Ndungulile alisema Serikali inafanya jitihada kubwa kwa kushirikiana na wananchi kuhakikisha inaimarisha afya za wananchi hivyo akaeleza kuwa juhudi hizo bila watumishi wa afya wa kutosha hazitakuwa na maana.
Alisema kwa sasa juhudi kubwa zimeelekezwa kwenye ujenzi wa vituo vya Afya na zahanati nchini ikiwa ni harakati za kuimarisha afya ya msingi kwa wananchi wake.
Naye Ofisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Mbeya, Aika Temu, alisema kada hiyo hapa inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa watumishi na hivyo kufifisha jitihada za kuhamasisha wananchi kwenye shughuli za maendeleo.
Alisema mkoa mzima wa Mbeya wenye wilaya tano na halmashauri saba una maofisa ustawi wa jamii 39 pekee, hivyo akaomba pia Serikali kuimulika idara hiyo wakati wa kuajiri watumishi wapya.
No comments:
Post a Comment