Friday, 19 January 2018

Wenye mabasi wataka kumwona JPM



WAMILIKI wa mabasi yaendayo mikoani, wameomba kukutana na Rais John Magufuli kumweleza matatizo yanayowakabili ikiwamo  vipengele wanavyodai kuwa ni kandamizi katika kanuni mpya za leseni za usafirishaji.

Wamefikia hatua  hiyo baada ya kutofikia mwafaka katika kikao kilichofanyika jana  jijini Dar es Salaam kati yao  na maofisa kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa  Usafiri wa Nchi kavu na Majini (Sumatra), Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, na Jeshi la  Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani.

Akitangaza azimio hilo kwa niaba ya wajumbe waliohudhuria mkutano huo, Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi hayo (Taboa), Enea Mrutu, alisema wataandika barua kuomba kukutana na Rais  Magufuli ili kumweleza matatizo yanayowasibu.

"Tukimaliza kikao hapa na kwa kuwa wote mmekubali na mnataka kukutana na Rais  Magufuli, sekretarieti itakutana tutaandika hiyo barua na tutaipeleka nyumba nyeupe (Ikulu)," alisema Mrutu.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Taboa , Mohammed Hood, alisema kabla ya kuandikia barua ya kuomba kukutana na Rais, watafanya utaratibu wa kuonana na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa.

"Hatuwezi kufika kwa Rais  moja kwa moja bila  kupitia kwa Waziri, hivyo mimi  nitampigia Waziri ili nimwombe tuonane na baada ya hapo ndipo  tutakwenda  Ikulu," alisema Hood.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa Barabara, Johansen Kahatano, alisema hakuna uadui kati ya Sumatra na wamiliki wa mabasi na kwamba suala la faini inayotozwa kuanzia Sh. 250,000 hadi 500,000 haliwezi kuingiliwa kwa sasa kwa sababu ni la  kisheria.

"Jambo hili litafutiwe namna nyingine ya kuzungumza kwa sababu lipo kisheria. Hakuna mmiliki atakayeshitakiwa  au kupelekwa mahakamani kwa kosa la  gari kwenda kasi, dereva ndiye atakayeshitakiwa," alisema Kahatano.

Kahatano aliwataka Taboa kwenda Tume ya Ushindani kulalamika endapo wanaona kanuni au sheria hizo mpya zinawakandamiza.

Kuhusu  kuzuia gari kwa kosa la  dereva, Kahatano alisema sheria ya Sumatra inasema endapo gari litakamatwa, mmiliki wa gari atapewa siku 14 za kulipa faini hiyo na endapo siku hizo zikipita bila kulipa, mmiliki anaweza kufika Polisi au Sumatra na kutaka kesi iende mahakamani.

Alisema hakuna gari lolote litakalozuiwa kwa kosa alilofanya dereva na kwamba makosa ya dereva na mmiliki yametenganishwa.

Wakichangia katika mkutano huo, wajumbe wa Taboa wengi wao  walilamikia kanuni zilizokuwapo katika leseni za usafirishaji kuwa zinawakandamiza, huku wakipendekeza faini za viwango vipitiwe upya pamoja na makosa ya dereva na mmiliki yatenganishwe.

Source: Nipashe

No comments:

Post a Comment