Saturday, 20 January 2018

RIPOTI MAALUM: NI KWELI KUNA DAWA ZA KUONGEZA NGUVU KIUME -3


MSOMAJI,bado naendelea kukufungua ufahamu kuhusu suala la tatizo la upungufu wa nguvu za kiume. Wiki iliyopita tuliona jinsi wataalamu walivyoelezea mishipa ya damu inavyosababisha ukosefu wa nguvu za kiume kama ina hitilafu. Tuliona pia jinsi moyo ukiwa na hitilafu unavyosababisha mwanaume kukosa nguvu hizo za kufanya tendo la ndoa, endelea sehemu hii ya tatu ambayo inajikita zaidi na virutubisho katika mwili vinavyosaidia kumpa nguvu yule ambaye hana nguvu za kiume.
Endelea: Toleo lililopita tuliona kuwa upungufu wa nguvu za kiume unasababishwa na mambo mengi kama vile mishipa ya damu kuwa na kasoro lakini leo tutafafanua kuhusu ukosefu wa virutubisho muhimu mwilini na jinsi ya kuongeza nguvu za kiume bila kutumia dawa za viwandani.

Ni jambo muhimu kama mtu atazingatia kula vizuri na kufanya mazoezi ili kuthibiti nguvu za kiume. Mazoezi yapo ya aina nyingi, kwa wale wenye umri mkubwa wanaweza kufanya mazoezi ya kutembea kwa mwendo wa kasi kwa dakika 35 au saa nzima kila siku. Wakati mwingine pia wanaweza kufanya mazoezi ya kukimbia kwa zaidi ya dakika 30, kuogelea au mazoezi ya kufanyia kwenye vyumba maalum vya mazoezi(gym), kufanya jogging mkiwa katika makundi au mmoja mmoja.

Mazoezi ni tiba ya vitu vingi mwilini ikiwa ni pamoja kuondoa presha na kwa wale wenye matatizo ya nguvu za kiume. Ili kuongeza nguvu za kiume si lazima kutumia dawa kali kama viagra au vilevi vikali. Dawa na pombe hukupa nguvu zinazodumu na kuisha kwa muda mfupi, lakini hukuletea madhara makubwa yatakayoathiri mwili kwa muda mrefu zaidi.

Ili kupata suluhisho la uhakika la nguvu za kiume Mtaalamu wa Lishe, Abdallah Mandai anasema ni vizuri kuzingatia vyakula vinavyoweza kukuongezea stamina na kujenga mwili wako vizuri na kukupa uwezo wa kufanya mapenzi vizuri zaidi bila kutumia dawa; vyakula ni suluhisho maridhawa kwa kila kitu maishani mwako. Anasema mwili wako una maarifa ya kujirekebisha pasipo kuhitaji dawa au vilevi, unachotakiwa kuzingatia ni chakula bora tu.

Sehemu za viungo vya uzazi kwa mwanaume kutokuwa na kiwango cha kutosha cha homoni ya Testosterone, kupungukiwa protini na hivyo kukosa amino asidi mwilini na kusababisha ukosefu wa nguvu za kiume. Leo napenda tuangalie vyakula ambavyo vinasaidia kuongeza na kuboresha nguvu za kiume na kusaidia kwa kiasi kikubwa kudumisha mapenzi na kulinda uhusiano na ndoa, hivyo hii ni dawa nzuri ya asili ya kurejesha nguvu za kiume.

Matunda ambayo husaidia kuondoa tatizo hilo ni haya yafuatayo:
BLUEBERRY Blueberry ni matunda yanayosaidia sana kuongeza nguvu za kiume, wengi hupendelea kuyaita ‘viagra’ asilia kutokana na kazi nzuri inayoifanya mwilini ya kuongeza nguvu za kiume. Kama tulivyoona wiki iliyopita kuwa mishipa ya damu ni muhimu, Mtaalamu wa Lishe, Abdallah Mandai anasema, blueberries ina virutubishi vinavyoimarisha mishipa ya damu na kusaidia mzunguko mzuri wa damu mwilini, niwakumbushe tu kuwa damu ndiyo kila kitu katika nguvu za kiume.

Anasema blueberries zina nyuzinyuzi (fiber) ambazo husaidia kuondoa kolesteroli (Cholestrol) mwilini kabla hazijanganda kwenye mishipa ya damu. Kuwa na mzunguko mzuri wa damu husaidia mwanaume kuwa na nguvu za kiume hivyo kuhimili kufanya mpenzi wa muda mrefu zaidi. “Kuna matunda yanayoitwa mtini (figs); ni matunda yenye kiwango kikubwa cha amino asidi, ambayo ni kiungo kikubwa katika kuzalisha homoni mwilini. Homoni ndiyo kishawishi cha nguvu za kiume mwilini. Kukosa amino asidi huweza kusababisha kukosa hamu ya mapenzi au kupungukiwa na nguvu za kiume,” anasema Mandai.

CHAZA/KOMBE (RAW OYSTERS)
Anaongeza kusema chaza wana kiwango kikubwa
cha madini ya zinc. Madini za zinc hutumika katika utengenezaji wa homoni ya testosterone, na mbegu za kiume. Uwingi wa uzalishwaji wa testosterone mwilini huathiri pia hamu ya mapenzi na nguvu za kiume ikiwa kidogo huondoa hamu, ikiwa nyingi humfanya mtu kuwa na hamu na nguvu zaidi. Kupungukiwa kwa madini ya zinc husababisha kupungua kwa nguvu za kiume, udhaifu na kushuka kwa kiwango cha uwezo wa kufanya ngono.
KARANGA
Mtaalamu huyo anasema, karanga ni chanzo kikubwa cha kujenga protini mwilini kwani huwa na kiwango kikubwa cha amino asidi ambayo husaidia kuweka vizuri mfumo wa damu, hivyo kusababisha kuongezeka kwa kiwango cha nguvu za kiume.

VITUNGUU SAUMU Anaongeza kuwa kitunguu saumu kina allicin, kiambato kinachosaidia mzunguko mzuri wa
damu kwenye viungo vya uzazi. Kuwa na mzunguko mzuri wa damu kwenye uume ni sababu kubwa ya kuongeza stamina ya kufanya mapenzi.

NDIZI Anasisitiza kuwa ndizi ni chanzo kikubwa cha vitamin B ambayo husaidia sana katika kuongeza stamina na nguvu mwilini hasa wakati wa kufanya kazi nzito. Ndizi ina kimeng’enyo cha Bromelain ambacho huongeza nguvu za kiume na ashki ya mapenzi (libido).
CHOCOLATE
Kuhusu chocolate mtaalamu huyo anasema inasaidia kuongeza stamina kwenye kufanya kwa sababu ina viambato vya phenylethylamine na alkaloid. Anasema Phenylethylamine ni kiambato kinachofanya mtu kujisikia vizuri, hasa wakati wa kufanya mapenzi na alkaloid huongeza stamina na nguvu za kiume.

Haishauriwi kutumia dawa kama Viagra kuongeza nguvu za kiume badala yake watu wanatakiwa kutumia njia asilia katika kutatua matatizo hayo ya kiafya. Mwili una njia zake za kurekebisha kila kitu. Ukiona kuna tatizo mwilini, inaashiria kuna upungufu ambao unatakiwa kurekebishwa.

Kutumia madawa makali hudhoofisha mwili na hivyo kuupunguzia uwezo wa kufanya kazi kama inavyotakiwa. Ni vizuri kama utamuona daktari kama ukiona hakuna kinachowezekana kabla hujaanza kutumia dawa za viwandani.

Mara nyingi njia asilia ya kutumia vyakula hutumia muda mrefu sana kuleta mabadiliko, lakini matokeo yake hudumu zaidi kuliko kutumia madawa makali ambayo hutibua mfumo wa kawaida wa ufanyaji kazi wa mwili wako.

Ni vizuri kula kwa kiasi kabla ya kufanya mapenzi, hasa wakati wa usiku kabla ya kwenda kulala. Ni vizuri ukajaribu kubadilisha chakula unachokula, fanya mazoezi mara kwa mara ili kupata mwili wenye nguvu. Itaendelea wiki ijayo.
Na Elvan Stambuli

No comments:

Post a Comment