Saturday, 20 January 2018

FAHAMU MAKUNDI YA VYAKULA MUHIMU MWILINI



CHAKULA ni muhimu kwa maisha ya binadamu kwani humwezesha kupata nguvu na virutubisho ambavyo husaidia kuujenga mwili na kuupa kinga dhidi ya maradhi mbalimbali.

Kuna aina za vyakula ambavyo pia vina kazi tofauti mwilini na vina virutubisho tofautitofauti, hivyo mtu anatakiwa kula vyakula vya aina mbalimbali kwani aina moja haiwezi kuwa na virutubisho vyote vinavyohitajika mwilini.
Virutubisho vina kazi maalumu mwilini na hii huwezesha mfumo wa mwili kufanya kazi vizuri. Vyakula vimegawanyika katika makundi mbalimbali kulingana na kazi za vyakula hivyo mwilini.

Hata hivyo, vyakula vilivyo katika kundi moja huweza kuwa na aina ya viwango tofauti vya virutubisho na wakati mwingine hata aina ya virutubisho vilivyomo.
Kwa hali hiyo basi, mtu anatakiwa kula mchanganyiko wa vyakula mbalimbali ili kupata virutubisho vyote vinavyohitajika mwilini.
Mlo wenye mchanganyiko wa vyakula vyenye virutubishi vya aina zote, huitwa mlo kamili ambao ni muhimu sana hasa kwa watoto, ambao huwasaidia kukua vizuri na kuwa na afya njema.

Mlo kamili humwezesha mtu kujikinga na maradhi mbalimbali kama vile malaria, surua, kuharisha, shinikizo la damu, kisukari, magonjwa ya moyo na hata ukimwi.
Mlo kamili na wa kutosha hutoa virutubishi kama vile protini, vitamini, madini na nishati. Vile vile mlo kamili ni muhimu kwa wazee na wagonjwa katika kujenga mwili na kusaidia uponaji wa majeraha, na kupata nguvu baada ya kukabiliana na maradhi.
VYAKULA VYENYE WANGA
Vyakula vya wanga ni muhimu katika kuupa nguvu mwili za kufanya kazi mbali mbali.
Vyakula vyenye wanga ni nafaka, kama mahindi, mchele, ngano, mtama, ulezi, uwele na kadhalika.
Wanga pia hupatikana katika mihogo, viazi vitamu, viazi mviringo, viazi vikuu, magimbi, ndizi, miwa na asali.
 
VYAKULA VYENYE PROTINI
Protini ni muhimu sana katika kujenga mwili na kuwezesha ukuaji wa mwili hasa kwa watoto na pia husaidia kutengeneza kinga ya mwili.
Vyakula vyenye protini ni pamoja na nyama ya ng’ombe, mbuzi, kondoo, nguruwe, kuku, bata, samaki nk.
Protini pia hupatikana kwa kula mayai, maziwa na kunde, maharage, soya, dengu, choroko, njegere, mbaazi, na njugu mawe.
 
VYAKULA VYENYE MAFUTA
Vyakula vyenye mafuta huleta joto mwilini, na vile vile huleta nguvu mwilini na kulinda. Hulainisha ngozi na pia utando (membrane).
Mafuta hutokana na mimea na huwa yanauzwa madukani kama vile, mafuta ya karanga, alizeti, nazi, ufuta, korosho, mawese, mbegu za maboga, mbegu za pamba.
 
MATUNDA NA MBOGA
Matunda na mboga ni muhimu sana katika mwili, kwa vile vyakula hivi vina vitamini na madini mbalimbali ambayo ni muhimu mwilini.
 
Vitamini na madini huhitajika kwa kiwango kidogo sana, lakini ni muhimu kwa mwili kuweza kufanya kazi zake vizuri.
Upungufu wa vitamini na madini mwilini unaweza kusababisha hitilafu mbalimbali katika mwili na hata kusababisha kasoro zinazoambatana na maradhi mwilini.
 
VITAMINI
Kuna vitamini mbalimbali ambazo ni Vitamini A, Vitamini B, Vitamini C, Vitamini, D na nyinginezo.
Vitamini A ni muhimu katika ukuaji hasa kwa watoto na utengenezaji wa chembechembe za mwili.
 
Husaidia kuongeza kinga mwilini na kuwezesha macho kufanya kazi vizuri. Vitamini A ni muhimu katika kutunza ngozi.
Vitamini A, hupatikana katika matunda na mboga zenye rangi ya machungwa na manjano, kama vile karoti, viazi vitamu vya manjano, maembe, na nyanya. Pia hupatikana katika mboga za majani, maini na maziwa.
 
Vitamini A husaidia kuzuia magonjwa mbalimbali hasa yanayosababisha ngozi kubabuka hasa katika zile sehemu zinazopigwa na jua au kama chakula kinashindwa kusagika vizuri na kusababisha kuharisha.
Ukosefu wa vitamin B unasababisha beriberi, ugonjwa unaofanya mtu kupungua uzito, moyo unaweza kuwa mkubwa, miguu kuvimba na kujaa maji.
 
Ukosefu wa vitamini B pia unaweza kusababisha midomo kupasuka, na dalili nyinginezo. Hupatikana katika mboga za majani kama vile spinachi, mchicha, matembele na kadhalika.
Vitamini C ni muhimu mwilini, husaidia ukuaji, kuongeza kinga mwilini na kusaidia mwili kutumia madini ya chuma.
 
Hupatikana katika machungwa, limao, machenza, mananasi na mboga za majani ambazo hazikupikwa mpaka kuiva sana.

TU FOLLOW KWENYE MITANDAO YA KIJAMII 



No comments:

Post a Comment