KAMANDA WA POLISI MKOA WA KAGERA, AGUSTINE OLLOMI.
MWILI wa Betia Felix (18) mkazi wa Kijiji cha Nyakatete, wilayani Kyerwa mkoa wa Kagera, umeokotwa ukiwa umekatwa matiti na kufungwa kamba miguuni.
Marehemu huyo, alionekana kichakani Ijumaa iliyopita saa 4:00 asubuhi karibu na maeneo ya mashamba ya wanakijiji hicho baada ya ndugu kutokumwona nyumbani kwao kwa muda wa siku saba na kutoa taarifa ofisi za kijiiji.
Mwenyekiti wa kijiji hicho Josephat Mtayoba, alisema baada ya kupokea taarifa za binti huyo na kuwasiliana na ndugu wa marehemu walisema wakati akiondoka alikuwa anawasiliana na watu ambao ndugu zake hawakuwafahamu.
"Kwa kijiji hiki ni tukio la kwanza kushuhudia mauaji ya kushtua kama hatua zinazoendelea kuchukuliwa ni kuweka na kuimarisha ulinzi shirikishi, "alisema Mtayoba.
Baba wa marehemu huyo Felix Gabriel , alisema binti yake, alitoka shambani akiwa na jembe na kuliweka nyumbani kisha kuondoka akiwa anaongea na simu, lakini hakufahamu alikuwa akiongea na nani.
Aidha alisema baada ya kukaa kwa muda mrefu akiwa haonekani nyumbani alidhani kuwa mwanae atakuwa ameolewa hivyo anasubiri kupokea mahari kutoka kwa wakwe.
“Aliondoka nyumbani tangu Januari 5, mwaka huu na mwili wake kuokotwa na mdogo wake mchunguzi Felix Ijumaa iliyopita Januari 12 mwaka huu,”alisema Gabriel.
"Nilivyoona anaondoka sikushtuka kwani nilijua atarudi na alivyokaa siku nyingi nilidhani atakuwa ameolewa nilijipanga kupokea mahari ya binti yangu, "alisema Gabriel kwa uchungu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Agustine Ollomi, alithibitisha tukio hilo na kusema kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kuwatafuta wahalifu hao na kwamba hakuna aliyenaswa.
No comments:
Post a Comment