TUNAENDELEA kuchambua matatizo ya moyo na namna yanavyoweza kusababisha vifo.
Wiki iliyopita tulizungumzia ugonjwa wa mshtuko wa moyo, na tulieleza dalili za ugonjwa huo na makundi ya watu yaliyo kwenye hatari ya kupatwa na mshtuko wa moyo au heart attack.
Leo tutaendelea kuzungumzia ugonjwa huo na tutaelezea namna ya kutibu mshtuko wa moyo na namna ya kujikinga na ugonjwa huo; endelea.
FAHAMU NAMNA YA KUTIBU MSHTUKO WA MOYO
Mshtuko wa moyo unahitaji kushughulikiwa haraka. Kama unamshuhudia mtu akipatwa na mshtuko wa moyo unapaswa kuomba msaada haraka au kumfikisha kituo cha afya haraka iwezekanavyo.
Kama mtu aliyepatwa na mshtuko wa moyo amepoteza fahamu, baada ya kuomba msaada kituo cha afya cha karibu, unapaswa kumfanyia CPR mara moja kama unajua kufanya hivyo.
CPR ni kitendo ambacho husaidia kufikisha hewa ya oksijeni katika ubongo.
Kwanza hakikisha njia za hewa za mgonjwa ziko wazi, yaani hakikisha mdomoni na puani kwake hakuna kitu kinachozuia hewa kupita na msaidie kwa hewa kila baada ya kumkandamiza kifuani au (chest compress) mara 30.
Kama hujuia CPR pia unapaswa kuanza kumkandamiza kifuani mgonjwa aliyepoteza fahamu kutokana na mshtuko wa moyo, kwani kufanya hivyo huenda kukaokoa maisha yake.
Tutaelekeza hapa namna ya kumkandamiza kifuani mgonjwa aliyepatwa na mshtuko wa moyo na aliyepoteza fahamu.
Weka kiganya cha mkono wako mmoja katika mfupa wa kifua (chestbone) katikati ya matiti na kiganya cha pili juu ya cha kwanza, na kandamiza kwa kiasi cha inchi mbili au sentimeta 5 kuelekea chini. Eendelea kukandamiza na kuachia mara 30.
Kama unajua namna ya kufanya CPR mfanyie mgonjwa na kama hujui endele kumkandamiza sehemu hiyo ya kifua hadi msaada utakapowasili au hadi mgonjwa atakapopata fahamu au kuonyesha dalili za kupumua.
Matibabu ya ugonjwa wa mshituko wa moyo hufanyika hospitali kwa njia tofauti kulingana na hali ya mgonjwa.
Kila dakika inavyopita baada ya kutokea mshituko wa moyo, ndivyo tishu ya moyo inavyopoteza oksijeni na kuharibika au kufa.
Njia kuu ya kuzuia moyo usiharibike ni kurejesha tena haraka mzunguko wa damu.
Mgonjwa wa mshtuko wa moyo huweza kutibiwa kwa dawa au njia nyinginezo za tiba kwa kutegemea namna gani tishu ya moyo ilivyoharibika.
Dawa tofauti zinazotumika kutibu mshituko wa moyo ni kama aspirin, dawa zinazoyeyusha damu ili kuondoa damu iliyoganda ambazo huitwa kitaalamu kama clot buster, dawa aina ya heparin na nyinginezo ambazo hutofautiana kutokana na utendaji wake mwilini.
Baadhi ya wakati athari za mshituko wa moyo huwa kubwa ambapo mgonjwa hutibiwa kwa njia inayoitwa Angioplasty.
Hiyo siyo operesheni bali ni matibabu ya kufungua mishipa ya damu iliyoziba au kudhoofika na kusabisha mshituko wa moyo. Mara nyingine wagonjwa wa heart attack hutibiwa kwa upasuaji unaoitwa bypass surgery.
Baada ya kujua namna ya kutibu mshituko wa moyo, sasa tuangalie ni jinsi gani tunaweza kujiepusha na ugonjwa huo wenye madhara makubwa kwa miili yetu.
Kwa wale ambao tayari wameshapatwa na ugonjwa huu pia wanashauriwa kuendelea kutumia dawa walizopewa hospitalini lakini pia kubadilisha mienendo ya maisha yao ili kuzuia kupatwa tena na mshituko wa moyo katika siku zijazo.
Itaendelea wiki ijayo.
No comments:
Post a Comment