Friday, 19 January 2018

Waziri Mkuu Majaliwa ajitwisha mgogoro wa Nyamongo


Mapokezi ya mabango yaliyobebwa na wananchi wa eneo la Nyamongo yamesababisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kujitwisha mgogoro uliodumu kwa zaidi ya miaka 15 kati ya wakazi hao na Mgodi wa Dhahabu Acacia North Mara.

Serikali imeahidi kutatua mgogoro huo kati ya mgodi na wananchi wanaozunguka eneo hilo, ili kumaliza uhasama na kurejesha amani kati ya makundi hayo mawili yanayohasimiana kwa kipindi kirefu.

Ahadi hiyo ilitolewa jana na Majaliwa alipotembelea eneo la Nyamongo wilayani Tarime katika ziara yake ya siku saba inayoendelea mkoani Mara.

Hiyo ni baada ya kupokewa na mabango aliyosema hayapungui 400 alipofika eneo la Nyamongo, jambo alilosema ni ishara tosha ya kuwapo tatizo linalowachukiza wananchi linalohitaji ufumbuzi wa Serikali na viongozi wa ngazi zote.

Kikao cha kwanza cha kujadili na kutafutia ufumbuzi mgogoro huo kitakachohusisha wajumbe watano wa watakaowakilisha wananchi, uongozi wa mgodi, mbunge wa Tarime vijijini (John Heche) na wataalami wa Wizara ya Madini kitanatarajiwa kufanyika mjini Dodoma Januari 27.

Mambo muhimu yatakayojadiliwa na kupatiwa ufumbuzi kwa mujibu wa Waziri Mkuu ni malipo ya fidia kwa mali ya wananchi, maeneo ya uchimbaji kwa wachimbaji wadogo, upatikanaji wa mawe (mabaki) ya dhahabu maarufu kama magwangala.

Mengine ni upatikanaji wa maji safi na salama eneo la Nyamongo (vyanzo vya maji vya asili vinadaiwa kuchafuliwa na kemikali), na udhibiti wa matumizi ya nguvu kupita kiasi, ikiwamo kupiga mabomu ya machozi na risasi panapotokea mgogoro au vurugu kati ya wananchi na mwekezaji.

“Nimepokewa na mabango tangu nianze ziara mkoani Mara Januari 15; lakini mabango ya Nyamongo yametisha. Hayapungui 400 na yote yanaonyesha uhusiano mbaya kati yenu (wananchi) na mwekezaji. Nitalibeba hili na kulimaliza,” alisema Majaliwa akiamsha shangwe na nderemo kutoka kwa wananchi.

Licha ya amani na utulivu eneo la Nyamongo, uamuzi huo wa Serikali pia unalenga kuondoa kuviziana kati ya wananchi na vyombo vya dola vinavyotumika kudhibiti na kurejesha amani na utulivu nyakati za uvamizi unaofanywa na makundi ya watu, hasa vijana wanaoingia eneo la mgodi kuchukua mawe au mchanga wa dhahabu.

“Mgogoro huu unakwamisha juhudi za wananchi, Serikali na wawekezaji katika kujiletea maendeleo kupitia rasilimali ya madini yanayopatikana Nyamongo, lazima tuutafutie ufumbuzi wa kudumu kwa faida na masilahi ya pande zote,” alisema Majaliwa.

Alisema yeye binafsi ataongoza mazungumzo ya kutatua mgogoro huo hadi mwafaka utakapopatikana na kuagiza pande zote kuunga mkono juhudi hizo kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu huku maslahi na maendeleo ya wananchi yakipewa kipaumbele.

Awali, mbunge wa Tarime vijijini, John Heche alimweleza Majaliwa kuwa uhasama kati ya wananchi na wawekezaji, kukosekana kwa huduma bora za kijamii kulinganisha na ya utajiri wa madini eneo hilo na matumizi ya nguvu ya vyombo vya dola dhidi ya wakazi kwa faida ya mwekezaji bila kujali uhalali wa madai ya wenyeji ni miongoni mwa changamoto zinazowakabiliwa wakazi wa Nyamongo.



No comments:

Post a Comment